Na Sarah Moses, Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Patrobas Katambi amesema Serikali itaendelea kuwasaidia Wakulima kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika kilimo na kukwamisha uzalishaji bora wa mazao ya Mifugo na Kilimo.
Akizungumza Agosti 8 ,2023 jijini Dodoma katika kilele cha maadhimisho ya maonesho hayo yaliyoanza tangu Agosti mosi Mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine kulikuwa na utoaji wa tunzo kwa taasisi zilizofanya vizuri.
Amesema kuwa serikali itaendelea kuwasaidia Wakulima kwa kuboresha miundombinu ya kilimo ikiwemo kujenga mabwabwa ya umwagiliaji ambayo tayari Mhe. Rais ameshaanza kutoa Fedha za kujengea na mengine tayari yanatumika lakini pia ametoa mbolea za ruzuku kwaajili ya kuwapunguzia gharama Wakulima wetu”, amesema Katambi
Aidha Katambi amewataka Wakulima kutumia vizuri ardhi ya Tanzania kupitia teknolojia mbalimbali za kilimo ili waweze kuzalisha zaidi kwani ardhi hiyo inarutuba ya kutosha.
Kwa Upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa asilimia 72 ya wakazi wa Mkoa huo ni Wakulima na wafugaji hivyo wamedhamiria kujipanga vizuri katika Sekta hiyo.
“Mkoa wa Dodoma umedhamiria kujipanga katika Sekta ya kilimo na tunamshukuru Rais kwa kuendelea kutujengea mabwabwa ya umwagiliaji na Mkoa tunatarajia kujengewa visima 128 kwa Halmashauri zote za Mkoa huu ambazo zitarahisisha kilimo bila kutegemea mvua pekee,” amesema Senyamule
Hata hivyo naye Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida ametoa shukrani kwa wote walioshiriki katika maonesho hayo na kutoa elimu mbalimbali za namna ya kuongeza thamani ya mazao yatokanayo na Kilimo na Mifugo na kuwaomba waliopata Elimu hizo kuzitumia kwa vitendo ili ziwaletee manufaa.
Mwisho.