Yanga yapania kutetea Ngao ya Jamii

Na Asha Kigujndula

KLABU ya Yanga, imetamba itahakikisha inatetea ubingwa wao wa Ngao ya Jamii msimu wa 2023/24 katika michuano itakayofanyika kuanzia kesho jijini Tanga.

Michuano hiyo msimu huu inashirikisha timu nne za juu zitakazoanzia hatua ya nusu fainali ambapo Yanga itaumana na Azam FC huku Simba itaoneshana kazi na Singida Fountain Gate.

Yanga ikifanikiwa kutwaa taji hilo, itakuwa imetwaa kwa mara ya tatu mfululizo kwani msimu uliopita iliitandika Simba mabao 2-1, huku ule uliotangulia pia iliichapa Simba bao 1-0.

Akizungumza na gazeti hili leo kabla ya kuanza safari ya kwenda Tanga, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema wanakwenda Tanga kwa lengo moja tu kutetea taji lao.

“Tumedhamiria kushinda mataji yetu yote tuliyotwaa msimu uliopita na tunaanza na hili la Ngao ya Jamii, kikosi kimeondoka leo na tuna uhakika kikosi chetu kipo vizuri kupambana na kutupa matokeo mazuri,” ametamba Kamwe.

Kamwe amesema wachezaji wote kwenye kikosi cha timu hiyo wako katika hali nzuri na hakuna hata mmoja aliye na majeraha.

Amesema uongozi wa klabu hiyo chini ya Rais wao, Injinia Hersi Said umekuwa mstari wa mbele kuhamasisha na kuwaeleza wachezaji umuhimu wa kutetea taji hilo na kilichobaki ni upande wa wachezaji na benchi la ufundi kutekeleza dhamira hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *