Na Zahoro Mlanzi
HATIMAYE Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imeweka wazi ratiba ya msimu mpya wa mashindano wa ligi hiyo ambapo miamba ya soka hilo, Simba SC na Yanga SC, zitakutaka katika mzunguko wa kwanza Novemba 5.
Hata hivyo zitakata utepe wa ligi hiyo kwa mabingwa watetezi, Yanga kuanzia nyumbani kwa kuumana na KMC huku Simba ikiwa ugenini kuumana na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa kutangaza ratiba hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa bodi hiyo, Almasi Kasongo, anasema kama hakutakuwa na changamoto yoyote wana imani ligi hiyo itaanza Agosti 15 kama walivyotangaza na kumalizika Mei 29, mwakani.
“Mechi kubwa kwa maana ya Kariakoo Derby ya mzunguko wa kwanza itachezwa Novemba 5 ikiwa ni raundi ya nane, kati ya Simba na Yanga kuanzia saa 11 jioni Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam,” amesema Kasongo na kuongeza.
“Katika mechi za mzunguko wa kwanza msimu wa 2023/24, Simba itaanzia ugenini kuivaa Mtibwa Sugar huku Yanga ikianzia nyumbani kuumana na KMC kwenye Uwanja wa Azam Complex”.
Amesema mechi zitakazofungua pazia la ligi hiyo Agosti 15 ni kati ya Ihefu FC itakayoumana na Geita Gold, ikifuatiwa na mchezo kati ya Namungo FC na JKT Tanzania na mechi ya mwisho siku hiyo ni Dodoma Jiji itakayoumana na Coastal Union ya Tanga.
“Siku inayofuata ambayo ni Agosti 16 kutakuwa na michezo miwili kati ya Mashujaa FC ambayo imepanda daraja itakayoumana Kagera Sugar huku Azam FC ikiikaribisha Kitayoce ‘Tabora United’,” amesema Kasongo.
Pia Agosti 17 amesema kutakuwa na mchezo kati ya Mtibwa Sugar ambayo itaumana na Simba Uwanja wa Manungu Turiani ambapo siku inayofuata Singida Fountain Gate itaumana na Prisons ya Mbeya.
Pazia la raundi ya kwanza litafugwa Agosti 23 kwa Yanga kuumana na KMC mchezo utakaopigwa Uwanja wa Chamazi Complex.
Kasongo ameongeza ligi hiyo itamalizika Mei 29 kwa timu zote kucheza muda mmoja ambapo Simba itaumana na JKT, Coastal na KMC, Yanga itakuwa ugenini kuumana na Prisons, Singida na Kagera, Mashujaa itaikaribisha Dodoma Jiji, Azam itakuwa ugenini kuumana na Geita, Ihefu itaikabili Mtibwa na Namungo itaumana na Tabora United.