BERLIN, Ujerumani
BEKI Virgil van Dijk, amechaguliwa kuwa nahodha mpya wa timu ya Liverpool baada ya kuondoka kwa Jordan Henderson, imetangaza klabu hiyo ya Ligi Kuu England.
Nyota huyo, 32, alijiunga na miamba hiyo ya Anfield akitokea Southampton mwaka 2018 na ameshacheza mechi 222, huku pia akitoa mchango mkubwa kwa Taifa lake la Uholanzi.
Pia beki wa kulia, Trent Alexander-Arnold, amethibitisha ndiye atakayekuwa akimsaidia baada ya James Milner kuondoka na kujiunga na Brighton.
Henderson na Milner, waliondoka ndani ya klabu hiyo ikiwa ni katika kufanya maboresho eneo la kiungo ili kuwa na timu mpya kutokana na msimu uliopita kufanya vibaya na kumaliza nafasi ya tano katika Ligi Kuu England.
Hiyo ina maana timu hiyo imeshindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza tangu 2016.