BRISBANE, Australia
TIMU ya Zambia, imepata ushindi wake wa kwanza katika fainali za Kombe la Dunia kwa Wanawake baada ya kuitandika Coasta Rica mabao 3-1 katika mechi ya mwisho ya Kundi C.
Lushomo Mweemba, alifunga bao la kwanza kwa Zambia ndani ya dakika tatu za kwanza na Barbra Banda aliongeza la pili kupitia mkwaju wa penalti katika dakika 45 za kwanza.
Mchezaji wa Costa Rica, Melissa Herrera, alifunga bao la kufutia machozi baada ya mapumziko kabla ya Racheal Kundananji kufunga bao la ushindi dakika za lala salama.
Timu zote zilishatolewa katika mashindano hayo baada ya kucheza mechi mbili za awali.
Zambia ilifungwa mabao 5-0 na Japan na Hispania kila moja katika mechi za awali.
Timu hiyo imemaliza kwa kushika nafasi ya tatu kutoka kundi hilo mbele ya Costa Rica iliyoshika mkia.