FLORIDA, Marekani
MCHEZAJI mpya, Lionel Messi, ametambulishwa rasmi mbele ya mashabiki wa timu ya Inter Miami uwanjani DRV PNK.
Alitambulishwa mbele ya mashabiki 20,000 waliokuwa wakimsubiri kuweza kumuona mshindi mara saba wa Tuzo ya Ballon d’Or akiwa amepewa jezi namba 10.
Kwa ufupi wakati akizungumza katika lugha ya Kihispania, Messi, 36, aliwashukuru mashabiki hao waliojitokeza na kusema ana matumaini makubwa kama ilivyokuwa siku zote.
Mshindi huyo wa Kombe la Dunia akiwa na Argentina, amejiunga kucheza Ligi Kuu ya Marekani (MLS) kwa mkataba utakaomalizika mwishoni mwa 2025.
Nyota huyo anaungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Barcelona, Sergio Busquets, ambaye naye amesajiliwa na timu hiyo hadi 2025.
Pia Busquets, naye alitambulishwa rasmi katika usiku huo wa mwishoni mwa wiki.
Messi ameingia uwanjani kupitia mwambao mkubwa na kutambulishwa kama “Nambari 10 ya Marekani, nambari bora 10 zaidi ulimwenguni”.
Mshindi mara saba wa ‘Super Bowl’, Tom Brady na mshindi mara nne wa ubingwa wa NBA, Stephen Curry, pia walimkaribisha nyota huyo nchini hapa kupitia ujumbe wa picha za mnato.
“Kiukweli nataka kuanza matizi, nishindane,” amesema Messi. “Nina matarajio kama yenu mliyokuwa nayo ya kwamba siku zote ninashindana, kushindana kushinda, kuisaidia klabu kukua zaidi.”
Kamishna wa Ligi Kuu ya MLS, Don Garber, amesema kusajili mtu wa hadhi ya Messi na akichagua kucheza ligi hii ni “wakati wa mabadiliko”, na ana matumaini usajili huo utawafanya watu wengi kufuatilia ligi hiyo ulimwenguni kote.