LOS ANGELES, Marekani
MCHEZAJI nyota katika kikapu, LeBron James, amevunja ukimya kwa kusema ataendelea kuichezea timu yake ya Los Angeles Lakers msimu ujao.
James, 38, alisema ataendelea kucheza msimu wa 21 wa NBA na wa sita akiwa na Lakers baada ya kupokea Tuzo ya ESPY ya Kuvunja Rekodi Bora ya ufungaji vikapu iliyokuwa ikishikiliwa muda wote na Kareem Abdul-Jabbar katika NBA.
“Sijali ni kiasi gani ninaweza kufunga pointi au kipi naweza au siwezi kufanya uwanjani,” amesema LeBron.
“Swali la kuniuliza, je ninaweza kucheza bila kufanya udanganyifu? Siku ambayo sitoweza kujitoa kwa lolote uwanjani ni siku ambayo itakuwa nimestaafu. Mna bahati, siku hiyo sio leo.”
Mwishoni mwa msimu uliopita baada ya Lakers kupoteza mbele ya Denver Nuggets katika Fainali za Western Conference, LeBron alisema hana uhakika kama atarejea na timu hiyo.
Huo ndio utata wa kauli ya awali ya LeBron, wakati akirudia kauli hiyo kwa nyakati tofauti na kusema angependa kucheza na mtoto wake mkubwa wa kiume, Bronny katika NBA.
Nyota huyo, alikuwa na msimu mwingine mzuri 2022-23, akiwa na wastani wa pointi 28.9, ‘rebound’ 8.3 na asisti 6.8 katika michezo 55.