7 mbaroni utekaji Dar, kutaka dola milioni 3.5

Na Salha Mohamed, Dar es Salaam

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu saba wanaodaiwa kupanga njama, kumtishia kwa silaha, kumteka mkazi wa Masaki, jijini humo ambaye ni mwanamke Hani Nooh Hussein (29).

Watekaji hao walitaka kupatiwa dola za Marekani milioni 3.5 kutoka kwa baba wa mwanamke huyo ili wamuachie.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, alisema tukio hilo limetokea Oktoba 16, 2023, saa nne asubuhi wakati Hani akiwa anaendesha gari lake namba T.333 CHN Toyota Rav4.

Alisema ghafla akiwa eneo la Msasani Village alisimamishwa na sehemu ya kundi la watuhumiwa walioingia ndani ya gari lake.

Watekaji hao walimtisha Hani kwa silaha, kumteka na kuelekea maeneo ya Mbezi Beach, Mtaa wa Ujirani.

“Walimshikilia kwa nguvu siku nne wakidai fedha kwa vitisho kutoka kwa baba yake wakisema asipotoa dola za Marekani milioni 3.5 atapotezewa maisha,” alisema.

Baada ya polisi kupata taarifa ya tukio hilo, walifanya kazi ya ufuatiliaji wa kisayansi ambapo Oktoba 19, 2023 walifanikiwa kumuokoa mwanamke huyo, kuwakamata watekaji wote wakiwa na gari walilomteka nalo.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum limekamata silaha iliyotumika Pistol Glock 19 yenye namba LZB 614 iliyotengenezwa Austria ikiwa na risasi 4,” alisema.

Kamanda Muliro alitaja watuhumiwa ni Hassan Abusher Nur (39) Raia wa Canada mwenye asili ya Somalia, Mkazi wa Msasani, Nathan Lungumisa (27).

Wengine ni Fredick Chahonza (49), Assad Abdurasur (43), Fahad Mussa (32), Ilfan Saleh (41), pamoja na Nicolas Nilay (39).

Alisema jeshi hilo limekamilisha upelelezi wa tukio hilo na tayari watuhumiwa wote wamefikishwa kwenye Mahakama ya Kisutu kwa hatua zaidi za kisheria.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linaendelea kutoa onyo, halitosita kuchukua hatua za haraka kwa mtu au kundi lolote linalopanga au kujihusisha na vitendo vya kihalifu.

“Tunawaomba wananchi kuendelea kuchukia uhalifu na kutoa taarifa za wahalifu kwa Jeshi la Polisi ili ziweze kufanyiwa kazi haraka kabla ya mtukio,” alisema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *