Serikali kupanua wigo Uwekezaji wa Umma kupitia Sheria pendekezwa

Na Daniel Mbega,

Dar es Salaam

MAPATO ya Serikali yanaweza kuongezeka zaidi ikiwa Sheri mpya ya Uwekezaji wa Umma itapitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, Sheria hiyo itapanua wigo wa uwekezaji wa umma kwa Serikali, na hivyo kuongeza ukusanyaji wa mapato.

Kwa sasa, Serikali ina hisa katika jumla ya taasisi na kampuni 298, ambapo kati ya hizo 248 ni taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali na 50 ni zile ambazo Serikali inamiliki hisa chache.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba, kwa mwaka 2022/23, uwekezaji wa Serikali kwenye kampuni hizo zote ulikuwa jumla ya Shs trilioni 75.79.

Kwa upande wa mapato, katika kipindi hicho Serikali ilikusanya Shs trilioni 1.008 kutoka kwa kampuni 123 tu kati ya 298, kati ya hizo 15 ni zile ambazo Serikali ina hisa chache na 108 ni taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali.

Kwa maana hiyo, uamuzi wa Serikali kupitia Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji kuwasilisha Bungeni muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma mnamo Novemba 10, 2023 una maana kwamba, Serikali imedhamiria kupanua wigo wa uwekezaji na kuipa madaraka makubwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali pamoja na uwekezaji mwingine wa Serikali kwenye kampuni na taasisi zisizo za umma.

Chombo madhubuti

Dhamira hiyo njema ya Serikali inamaanisha kwamba, ikiwa muswada huo utapitishwa kuwa Sheria, Ofisi ya Msajili wa Hazina inaweza kubadilishwa jina na kuundwa kwa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma (Public Investment Authority – PIA) ili kuakisi majukumu na mwenendo wa ukuaji wa uchumi wa duniani. PIA itaendelea kusimamia utendaji wa taasisi zote za umma na kuwekeza katika taasisi na kusimamia uwekezaji huo, wigo ambao kwa sasa ni finyu.

Hii inamaanisha kwamba, kutakuwepo pia nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, ambaye pia atakuwa Mwenyekiti wa Bodi, atakayeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kama Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, alivyosema alipokutana na wahariri wa vyombo vya habari Jumanne, Novemba 28, 2023, lengo la Sheria hiyo mpya ni kuimarisha uwekezaji wa ndani wa Serikali, hususan kwenye mashirika na taasisi zake, ambako kimsingi uwekezaji ni mkubwa kulinganisha na mapato.

Kama nilivyosema hapo awali, uwekezaji wa Serikali upo katika taasisi na mashirika takriban 298, ambapo kati ya hayo, 248 ni taasisi, mashirika ya umma na wakala za Serikali ambapo zote ziko ndani ya nchi, na 50 ni kampuni ambazo Serikali ina hisa chache, kati yake 40 ziko ndani ya nchi na 10 ziko nje ya nchi.

Taasisi, mashirika na wakala za Serikali 213 zinajihusisha na utoaji wa huduma wakati 35 zinafanya biashara, wakati ambapo kampuni 50 zote ambazo Serikali ina hisa kidogo, zinajihusisha na biashara.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa mafanikio ya taasisi hizo na uwepo wa mfumo wa kisheria wa usimamizi wake, ufanisi na tija inayopatikana kutoka kwenye baadhi ya taasisi haukidhi malengo ya kuanzishwa kwake, hivyo Serikali haipati matokeo yanayotarajiwa ya uwekezaji wake.

Lakini pia kupitishwa kwa Sheria hiyo kutawezesha kuanzishwa kwa Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund – PIF) ambao utawezesha upatikanaji wa mitaji kwa wakati.

Kwa sasa, Sheria ya Mamlaka na Majukumu ya Msajili wa Hazina, Sura 370 haibainishi vyanzo vya fedha za mitaji kwa ajili ya uwekezaji katika Taasisi na maeneo mengine.

Faida za kuanzisha Mfuko wa Umma ni nyingi, lakini baadhi ni kwamba, Serikali itaweza kufanya uwekezaji wa kimkakati kwa wakati (Timely Strategic Investment Decision), itaongeza ufanisi wa uendeshaji (operational efficiency), itaokoa Mashirika ambayo bila Mfuko huo yanaweza kuanguka, na itawezesha Mashirika ya umma kustahimili ushindani.

Sheria hiyo pia inapaswa kuainisha vyanzo vya fedha za Mfuko, ambavyo vitakuwa ni pamoja na sehemu ya maduhuli yatakayokusanywa na Mamlaka, ambayo kiwango chake kitabainishwa kwenye kanuni.

Mfuko wa Umma utakapoanzishwa unapaswa kuwa chini ya uangalizi wa Kamati ya Uongozi ya Mfuko wa Uwekezaji wa Umma (Public Investment Fund Steering Committee) kwa kuzingatia miongozo itakayoainisha vigezo vya uwekezaji, ufuatiliaji pamoja na mambo mengine yanayohusu uendeshaji wa Mfuko.

Sheria hiyo inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kuidhinisha stahili za wajumbe wa Bodi za Taasisi, kwa sababu kwa sasa Msajili wa Hazina hana mamlaka ya kuidhinisha viwango vya stahili za wajumbe wa Bodi, na hivyo kushindwa kutoa motisha kwa Bodi zenye ufanisi na hivyo kuathiri utendaji.

Kwa hiyo, Mamlaka inapaswa kupewa mamlaka ya kuidhinisha stahili za Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi za Taasisi ili kuendana na majukumu, ufanisi na tija katika usimamizi wa uendeshaji wa Taasisi.

Sheria inayopendekezwa inapaswa kujumuisha majukumu yaliyorithiwa kutoka Consolidated Holding Corporation (CHC), ambayo yalihamishiwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kupitia Tangazo la Serikali Na. 203 la Mwaka 2014, haya hivyo hadi sasa majukumu hayo hayajajumuishwa kwenye Sheria.

Sheria inayopendekeza inapaswa kuipa Mamlaka ya Uwekezaji wa Umma, mamlaka ya kutoa miongozo ya usimamizi na uendeshaji wa Taasisi kwani kwa sasa Ofisi ya Msajili wa Hazina haina mamlaka ya kutoa miongozo ya kusimamia utendaji na uendeshaji wa Taasisi, bdala yake Msajili wa Hazina ana uwezo wa kutoa miongozo ya kiutumishi tu kwa mujibu wa Kanuni za utumishi wa umma.

Uimarishaji uwekezaji

Kufanikiwa kuimarika kwa uwekezaji kwenye taasisi za umma maana yake ni kwamba, taasisi na mashirika hayo yatapata faida na kuimarika, hivyo kuleta tija kwa Taifa.

Kimsingi, taasisi na mashirika yote ya umma, ambayo yako kwa mujibu wa sheria yakiwa chini ya wizara za kisekta ambako ndiko zinakopaswa kuwajibika, zinahitaji kuzalisha na kuleta tija kwa sababu mitaji ya mashirika na taasisi hizo inatokana na fedha za umma.

Kwa mujibu wa utaratibu wa kisheria, taasisi za umma ambazo zinazalisha na kuingiza faida, zinapaswa pia kupeleka gawio kwa Serikali kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina.

Kulingana na mfumo wa mizani ya Serikali, taasisi hizi zinachangia 17% ya wafanyakazi wote wa sekta ya umma wakati 83% ya ajira ni kutoka Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Aidha, taasisi hizo zinachangia wastani wa 90% ya mapato yote yakiwemo ya kodi (85%) na yasiyo ya kodi (15%), wakati ambapo Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zinachangia 10% ya mapato yote ya Serikali.

Kimsingi, wizara kwa aina ya kazi zake ni watumiaji na siyo wazalishaji, hivyo inawezekana kuongeza tija na mafanikio katika utendaji kazi wa taasisi hizo ili kuweza kumudu mahitaji ya Taifa.

Ikumbukwe kwamba, taasisi ni wazalishaji na zinapaswa kuzalisha kwa ajili ya kugharamia mipango yao binafsi na ya Serikali kwa ujumla.

Hii ni kwa sababu, kwa sasa matumizi yanaonekana kuwa makubwa kuliko mapato, jambo ambalo ni mzigo mkubwa kwa Serikali ingawa inawekeza.

Kwahiyo, ufanisi wa taasisi hizo unatokana na usimamizi thabiti wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo ina jukumu kubwa la kuzisimamia katika msuala yote ya utendaji.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, ujio wa muswada wa Sheria ya Uwekezaji wa Umma ya mwaka 2023 haukuja vivi hivi, bali umetokana na jitihada za Serikali za kutatua changamoto mbalimbali za usimamizi na uendeshaji wa taasisi hizo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kwamba, Serikali iliunda Timu ya Wataalamu kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kina wa mfumo uliopo sasa wa usimamizi na uendeshaji, ambapo ilishauri namna bora ya kusimamizi taasisi hizo kwa kuzingatia mazingira na mahitaji ya sasa.

Aidha, uchunguzi unaonyesha kuwa, Timu hiyo ilifanya uchambuzi kwa taasisi na mashirika yote yakiwemo yale ambayo Serikali ina hisa kidogo, ikiwa ni pamoja na kubainisha taasisi na mashirika yanayotoa huduma na yanayofanya biashara, au yanayofanya biashara na kutoa huduma kwa wakati mmoja.

Jambo jingine lilikuwa kubainisha taasisi ambazo kulingana na majukumu yake zinaweza kuunganishwa au hazihitajiki tena na hivyo kufutwa, kubainisha taasisi na mashirika ambayo kutokana na majukumu pamoja na umuhimu wake yabakie chini ya uangalizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina na yapi yawekwe kwenye utaratibu tofauti wa usimamizi.

Uchambuzi muhimu zaidi ni kwamba, ilitakiwa kubainisha namna bora ya usimamizi wa utendaji wa taasisi hizo kwa kubainisha ni maeneo gani yanaweza kupewa uhuru wa kujiendesha.

Timu hiyo ilichambua namna ya kuiboresha Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambayo ndiyo yenye dhamana kubwa katika kusimamia taasisi na mashirika hayo.

Ni muhimu kutambua kwamba, kwa hali ilivyo sasa, na mazingira ambayo Serikali imeyaweka, lazima uwekezaji ukue ili kuongeza mapato.

Lakini pia ukuaji huo unamaanisha kwamba kutakuwa na ongezeko la ajira na uchangiaji katika huduma na bidhaa pia utaongezeka.

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, uwekezaji wa Serikali unaongezeka kila mwaka lakini ufanisi wa mapato haulingani kabisa na uwekezaji huo.

Siyo siri kwamba, ufanisi na tija inayopatikana kutoka baadhi ya taasisi haukidhi kabisa malengo ya uanzishaji wake na Serikali, kwa kifupi, haipati matokeo yanayotarajiwa kwenye uwekezaji wake.

Inawezekana kabisa hii inatokana na upungufu uliomo katika Sheria ya Msajili wa Hazina, ambapo pamoja na mambo mengine, inakosa kifungu mahsusi kinachompa Msajili wa Hazina mamlaka ya kuwekeza katika maeneo kadha wa kadha, hususan maeneo ya kimkakati ili kuendana na mazingira ya sasa na mabadiliko ya kiuchumi duniani.

Lakini mapungufu mengine ni kukosa mamlaka ya kusimamia masuala muhimu kwenye uendeshaji wa Taasisi ili kupata matokeo chanya katika ufanisi na utawala bora kama vile Ofisi ya Msajili kutokushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uteuzi wa wajumbe wa Bodi na watendaji wakuu wa taasisi hizo.

Uchunguzi unaonyesha pia kwamba, hakuna chanzo cha uhakika na endelevu cha mitaji ya uwekezaji kwenye taasisi hizo na uendeshaji wa shughuli za ofisi, pamoja na wigo finyu wa uwekezaji ambao kimsingi unaathiri uwezo wa Serikali kupata na kutumia fursa za uwekezaji zinazojitokeza kwa wakati.

Ikiwa itakuwepo Sheria madhubuti ya Uwekezaji wa Umma, ni wazi kwamba kutakuwepo na muundo mpya wa taasisi husika au uimarishaji wake pamoja na kuwepo kwa Mfuko wa Uwekezaji, ambao utaipunguzia mzigo Serikali kwa namna moja au nyingine.

Jambo muhimu hapa ni kwamba, Sheria hiyo ya Uwekezaji wa Umma lazima impe mamlaka Msajili wa Hazina katika usimamizi pamoja na mambo mengine, hali ambayo italeta ufanisi mkubwa na matokeo chanya.

Sheria hiyo lazima ibainishe mamlaka ya kusimamia masuala muhimu ya uwekezaji kwenye taasisi na kiwepo chanzo cha uhakika na endelevu cha mitaji ya uwekezaji.

Aidha, Sheria hiyo inapaswa pia kuwa na kipengele cha masharti ya uwajibikaji kwa Msajili wa Hazina na iondoe mwingiliano wa kimamlaka katika kutoa maelekezo ya jumla au mahsusi kwa taasisi.

Ni kwa namna hii ndipo uwekezaji huu muhimu utaleta tija na manufaa kwa taifa na kuyafikia malengo ambayo Rais Samia anataka kuyaona.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *