NBC, JUBILEE ALLIANZ KUWAJENGEA UWEZO WAKANDARASI ZANZIBAR

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), kwa kushirikiana na Kampuni ya Bima ya Jubilee Allianz Tanzania, wameendesha semina maalum kwa wakandarasi wa Zanzibar wakilenga kuwajengea uwezo zaidi wakandarasi hao ili waweze kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo visiwani humo kwa ufanisi zaidi kupitia huduma  bora za kifedha na bima zilizobuniwa mahususi kwaajili yao.

Warsha hiyo iliyofanyika le Zanzibar ambapo imeongozwa na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Zanzibar Dkt. Khalid Salum Mohamed na kuhusisha uwepo wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Habiba Hassan Omar, wakandarasi, maofisa wa benki ya NBC wakiongozwa na Mkuu wa Madeni na Masoko ya Mitaji wa benki hiyo, Zuber Masabo, pamoja na maofisa wa kampuni ya Jubilee Insurance wakiongozwa na Mkuu wa Idara ya Uhakiki, Yassin Ally Masenza.

Akizungumzia hatua hiyo, Dkt Khalid pamoja na kuzipongeza taasisi hizo warsha hiyo muhimu, alisema hatua hiyo kwa kiasi kikubwa itaisaidia serikali kufanikisha kwa urahisi dhamira yake ya msingi ya ujenzi wa miundombinu visiwani humo, kwa kuwa miradi mingi inatekelezwa na wakandarasi wazalendo ambao baadhi yao bado wanakabiliwa na changamoto ya rasilimali fedha na ukosefu wa huduma sahihi za bima kwenye miradi yao.

“Zanzibar kwa sasa imeweka vipaumbele vikuu vinne; miundombinu ya usafiri na uchukuzi, uchumi wa buluu, huduma za kijamii kama elimu, afya, maji safi na salama, umeme pamoja na utalii. Utekelezaji wa miradi yote inayogusa maeneo hayo unahitaji rasilimali fedha ya uhakika pamoja na kinga yanapotokea majanga ya asili kama mafuriko, moto na vimbunga. Jitihada hizi za wadau hawa  wawili  zitasaidia kuwajengea uelewa na kufungua fursa kwa wakandarasi wetu ili wawe na majibu sahihi katika kufanikisha miradi hii kwa wakati na kwa ufanisi zaidi,’’ alisema Dkt Khalid.

Dkt. Khalid alielezea kuridhishwa kwake na ushirikiano unaoendelea baina ya serikali na mashirika na taasisi binafsi katika kufanikisha miradi mbalimbali kwa maendeleo ya Taifa.

“Hivyo ni matumaini yetu kuwa baada ya semina hii wakandarasi wetu hususani wazalendo watanufaika na elimu hii na wataitumia kama chachu katika kufanikisha utekelezaji wa miradi kwa viwango vya juu zaidi. Serikali kama mdau wao mkubwa zaidi tunahitaji kuona miradi yetu inatekelezwa kwa ubora unaozingatia thamani ya fedha na muda,” ameongeza Dkt. Khalid.

Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Masabo alisema benki hiyo imejipanga kutoa huduma mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wakandarasi wa ndani kupata fedha na usaidizi wa kifedha kwa urahisi, kwa lengo la kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundobinu kwa wakati na ubora uliokusudiwa.

“NBC tunatambua kuwa maendeleo ya sekta ya ujenzi ni kichocheo kikuu cha maendeleo ya taifa. Na hili kufanikisha hili ni lazima wakandarasi wetu hususani wazalendo wawe na uwezo mkubwa kifedha ili waweze kushindana na wenzao kutoka nje ya nchi. Pamoja na mafunzo haya kuhusu huduma zetu mahususi kwao, tumejipanga zaidi kwenye kutoa huduma bora na rafiki kwa wakandarasi ili waweze kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo,” amesema Masabo.

Masabo ametaja baadhi ya huduma zinazotolewa na benki hiyo kwa wakandarasi kuwa ni pamoja na dhamana na mitaji  (Working capital guarantee facilities) kwaajili ya kuombea zabuni mbalimbali, mikopo ya muda mrefu ya zaidi ya miaka mitano hadi saba, Uhandisi na Ununuzi pamoja na Ufadhili (EPC +F), na kutoa mikopo kwenye miradi ya ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki wa Bima kutoka Jubilee Allianz Tanzania, Yassin Ali Masinza, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na benki ya NBC na wakandarasi kwa kutoa huduma za bima zinazowalinda dhidi ya hatari na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa miradi yao mbalimbali

“Tumejifunza kuwa changamoto kubwa kwa wakandarasi ni upatikanaji wa huduma za bima kwa wakati na kwa gharama nafuu. Jubilee Insurance tupo tayari kuandaa bidhaa maalum zinazolenga mazingira ya wakandarasi wa Zanzibar,” amesema Masinza.

Warsha hiyo ilihitimishwa kwa mijadala ya wazi ambapo wakandarasi walipata fursa ya kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na kupata mrejesho kutoka kwa wataalamu wa NBC, Jubilee Insurance na taasisi nyingine washirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *