Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
KUANZIA jana Jumatatu, Juni 24, 2024, wafanyabiashara wa eneo maarufu la Kariakoo jijini Dar es Salaam wameanza mgomo huku wakisema hawatafungua biashara mpaka madai yao yatakapotimizwa.
Na mgomo huu unafuatia vipeperushi vilivyoanza kusambazwa kuanzia Juni 22, 2024 kupitia mitandaoni vikielezea kusudio la mgomo huo, huku Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Kariakoo, Martin Mbwana, akinukuliwa akisema kwamba hizo ni hasira za kuchoshwa na mambo wanayofanyiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mbwana mwenyewe akakiri kwamba, wamekutana na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba, na kuwasihi wafanyabiashara kuwa watulivu kwamba tamko lingetoka jana, lakini wafanyabiashara hao wakaamua kutekeleza azma ya mgomo hata bila kusubiri tamko hilo.
Hamisi Livembe, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT), juzi Jumapili alinukuliwa akikanusha taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba kuna mgomo wa wafanyabiashara.
Livembe akasema, jumuiya hiyo haijakaa kikao chochote kilichoazimia kuitisha mgomo huo.
“Tangazo la mgomo kwa wafanyabiashara linalosambaa kwenye mitandao halijatoka kwenye Jumuiya yetu, tumewasiliana na mikoa yote na maeneo ya kibiashara, Kariakoo na viongozi wote wanasema hawajatoa hilo tangazo,” akasema Livembe.
Akasema, licha ya wafanyabiashara hao kuwa na malalamiko ya baadhi ya hoja za kikodi siku za karibuni, viongozi wa jumuiya hiyo wakiongozwa na yeye mwenyewe walikwenda jijini Dodoma (ambako bado wako mpaka sasa) kwa ajili ya kujadiliana na serikali.
Livembe akasema, baada ya mazungumzo ya pande mbili hatimaye muafaka ulifikiwa, na kwamba uamuzi uliofikiwa utatangazwa na Waziri wa
Fedha, Dkt. Nchemba, wakati akihitimisha Hoja ya Bajeti Kuu ya Serikali Bungeni leo hii.
Akasema, baada ya viongozi hao kupata taarifa za uwepo wa vipeperushi na matangazo yanayosambaa mitandaoni kuhusiana na mgomo, waliamua kuwasiliana na viongozi wote wa jumuiya hiyo kutoka kwenye mikoa na wilaya mbalimbali nchini, ikiwemo viongozi wa Soko la Kimataifa la Kariakoo, lakini kote walikanusha kuvitambua vipeperushi vya mgomo huo.
“Inawezekana tangazo hili limepenya kutoka nje ya Jumuiya yetu, inaonekana kama tumetunga sisi, sisi jumuiya hatuungi mkono hili,” akasema.
Lakini mbali na hayo, Livembe alifafanua kuwa wafanyabishara wote nchini
wanatambua njia na taratibu za kufuatilia mambo yao ikiwemo kufikisha kero na malalamiko yanayowakabili kwa viongozi wao.
Akasema, wafanyabiashara walitegemea mambo yanayowahusu kuwemo kwenye bajeti iliyosomwa Juni 13, 2024 na Waziri wa Fedha, ambapo hawakuridhishwa.
“Junii 19, 2024 tuliitwa na Serikali tukafanya vikao Juni 20 na 21, 2024, tumefikia makubaliano, katika makubaliano yale kuna vitu baadhi vimechukuliwa lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza za kimbunga, uharibifu wa mvua, serikali ina mahitaji makubwa ya fedha,” akasema.
Akaongeza kuwa, madai hayo yatasababisha kupunguza mapato ya serikali na kwamba zipo hoja ambazo zitaingia kwenye Bajeti ya mwaka huu.
Kulingana na Livembe, kulikuwa na hoja 21 za wafanyabiashara ambazo zikitatuliwa migogoro ya wafanyabiashara na serikali, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Halmashauri itakuwa imekwisha.
“Kuna jumla ya hoja 28 tulizoziwasilisha kwa Serika, hoja 12 zipo kwenye Kamati ya Waziri Mkuu na hoja 16 ni mpya. Katika hoja 14 walizoziainisha kwenye vipeperushi, ni hoja mbili pekee ndiyo ambazo Jumuiya inazijua, hizo nyingine hazijulikani,” akasema.
Yeye mwenyewe anashangaa haya mambo yametokea wapi, ikiwemo huo mgomo ulioanza jana, huku akisema, kuna vitu vipya ambavyo hawajawahi hata kuvisikia kwenye vikao vyao, kiasi kwamba wakati mwingine wanapata mashaka nani anavichochea.
Na anashangaa kwa sababu, anasema yapo mambo mengi ambayo serikali imekamilisha kwa wafanyabiashara ikiwemo hoja 9 zilizokuwa kwenye Kamati ya Waziri Mkuu ambazo zimeingia kwenye Bajeti ya serikali mwaka huu.
Kumbukumbu zilizopo zinaonyesha kwamba, Serikali imesitisha zoezi la ukaguzi wa Risiti za Kielekroniki (EFD) na ritani za kodi iliyokuwa ikifanywa na TRA kupitia Mkoa wa Kikodi wa Kariakoo, wakati ukiandaliwa utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hilo katika Soko Kuu la Kimataifa la Kariakoo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alikaririwa jijini Dodoma wakati akitoa maazimio ya kikao kati ya Viongozi wa Wafanyabiashara Tanzania, Viongozi wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo na Taasisi zinazosimamia masuala ya wafanyabiashara, kikao ambacho kiliitishwa na Waziri wa Fedha, Dkt. Nchemba na kuhudhiriwa pia na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.
Kama haya yalifanyika, mgomo unatoka wapi?
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, anasema “yawezekana wafanyabiashara wana malalamiko ya dhati kabisa, lakini masuala ya mgomo yasichukuliwe kuwa ni jambo la pamoja.”
“Kila mmoja awe na tafakari ya kutosha kabla hajafikia wazo hilo la kufunga biashara. Mtu yeyote ambaye anaweza kuleta ubabe na kutokusikilizana, maana yake serikali nayo inaweza kuamua kufanya hivyo hivyo, jambo ambalo si falsafa ya Rais,” akaonya Chalamila na kuwaasa wafanyabiashara wasigome, lakini wamekaidi.
Kama alivyosema RC Chalamila, wafanyabiashara wanaweza kuwa na hoja za msingi, lakini mgomo siyo njia sahihi ya kutatua changamoto zinazowakabili.
Swali la msingi la kujiuliza, ni nani aliye nyuma ya mgomo huu wa wafanyabiashara na lengo lake ni nini hasa?
Fikra mbadala zinahitajika hapa, kwamba, kama hoja tisa kati ya 12 ambazo zilikuwa katika Kamati ya Waziri Mkuu zilikwishapatiwa ufumbuzi, iweje leo hii wafanyabiashara waendelee kulalamika mambo yale yale ikiwemo suala la ulazima wa kusajili maghala yanayohifadhi bidhaa na kamatakamata ya TRA dhidi ya wafanyabishara na wateja kutoka nchi jirani wanaofanya ununuzi katika Soko la Kariakoo.
Walipogoma kwa siku tatu kuanzia Mei 15 – 17, 2023, hoja hizo zilizungumzwa na zikawekwa kwenye orodha ya kero za kushughulikiwa katika Kamati ya Waziri Mkuu, lakini bado zinaendelea kufukuliwa wakati zimefanyiwa kazi.
Hii ndiyo inayowafikirisha wengi, kwa sababu ni wafanyabiashara hao hao wa Kariakoo ambao mwezi Aprili 2024 walikuwa wanataka kuitisha mgomo na kuitingisha serikali, kabla ya mgomo huo kuyeyuka.
Na kwa wakati ule walikuwa wanalalamikia mambo matatu – suala la Wachina wanaofanya biashara pale, lile Soko Kuu la Kariakoo pamoja na Wamachinga.
Halafu wakaenda mbali kwa kugusia Soko la Kimataifa la Ubungo, ambalo kukamilika kwake kutakuwa na manufaa makubwa kwa wafanyabiashara wengi pamoja na wananchi kwa ujumla, kwani wafanyabiashara watakuwa wakinunua bidhaa hapo kwa bei nafuu kuliko gharama wanazoingia za kuagiza mizigo China na Dubai.
Nakumbuka katika moja ya vikao vyao, viongozi wa kitaifa wa JWT na wafanyabiashara hao walikubaliana kwamba, waunde kamati wakae na Wamachinga kwa kuwa ndani ya Soko la Kariakoo linalokarabatiwa kutakuwa na sehemu 1,500 ambazo watapewa Wamachinga, hivyo watatakiwa kwenda huko na siyo kupanga bidhaa barabarani na kusababisha usumbufu hata kwa wapitao.
Wachunguzi wanaeleza kwamba, wafanyabiashara wazawa wenyewe wamekuwa wadanganyifu kuhusu suala la wageni, hasa Wachina ambao waliambiwa inabidi wapate vibali vya kazi kutoka kutoka Wizara ya Kazi ndipo wakate leseni.
Lakini taarifa zinasema, mzawa anakwenda kukata leseni, halafu duka anamkabidhi Mchina kuliendesha. Kwa kifupi, anakuwa amempangisha Mchina badala ya yeye mwenyewe kufanya biashara.
Mamlaka zinapofanya msako na kuwabaini wageni wanaofanya biashara bila kufuata taratibu zinazotakiwa, ikiwemo kutokuwa na vibali vya kazi, wafanyabiashara wazawa ambao wananufaika na hujuma hizo, wanaanza kupiga kelele.
Kimsingi, hata huu mgomo waliouitisha una walakini na tafsiri ya wananchi walio wengi ni kwamba, huenda wafanyabiashara hao wanatumiwa na watu wengine ili tu kuiyumbisha serikali.