MIRADI YA TACTIC IMELETA MAPINDUZI YA KIUCHUMI MAJIMBONI KWETU- WABUNGE

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WABUNGE wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wameeleza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kijamii yaliyojitokeza ikiwamo fursa za kiuchumi inayotokana na kuboreshwa kwa mazingira ya ufanyaji wa biashara katika majimbo yao tangu kuanza kutekelezwa kwa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) kwa awamu ya kwanza na ya pili.

Jana Jumatano Juni 25, 2025 kwenye Mji wa Serikali, Mtumba Mjini Dodoma wakati wa utiaji saini utekelezaji wa miradi hiyo kwa miji 11 ya Tanzania bara, ambayo ni Morogoro na Songea kwa awamu ya kwanza pamoja na Miji ya Tanga, Korogwe, Babati, Shinyanga, Bukoba, Bariadi, Lindi, Iringa na Njombe, Wabunge wanufaika wa miradi hiyo wameeleza kuwa TACTIC imesaidia katika kuboresha usimamizi na ukuaji wa Miji sambamba na kuboresha utoaji wa huduma zinazotolewa na halmashauri zao kwa wananchi.

Mbunge wa Tanga Mjini Mhe. Ummy Mwalimu, miongoni mwa Viongozi wanufaika wa Ujenzi wa mifereji ya maji, taa za barabarani na barabara za lami, amebainisha pia kuwa ujenzi wa Soko la Makorora na Soko la Samaki la Deep Sea Mjini Tanga ilikuwa ni ndoto na kilio cha muda mrefu na kubainisha kuwa kukamilika kwake kutabadilisha hadhi na muonekano wa Mji wa Tanga na kuongeza kipato kwa wajasiriamali na wafanyabiashara wa Mji huo kutokana na mazingira yao ya biashara kuwa ya kisasa na yenye kuvutia.

Kwa upande wake, Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu, alibainisha kuwa kujengwa kwa soko la Kihesa kwenye mradi wa TACTIC awamu ya pili kutaondoa adha ya wajasiriamali kufukuzwa na Mgambo wa Mji kutokana na kufanya biashara maeneo yasiyokuwa rasmi katikati ya Mji pamoja na kukuza mzunguko wa fedha na uchumi wa Iringa Mjini.

Aidha, mbele ya mgeni rasmi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Msambatavangu pia alieleza kuwa ujenzi wa barabara ya Mkimbizi – Bima, Mtwivila, Viziwi na barababara ya Bontank kutainufaisha zaidi Iringa kiuchumi na Kiutalii na hivyo kupendezesha mandhari ya Mji wa Iringa pamoja na kuimarisha shughuli za kiutalii katika mji huo ulio kitovu cha utalii kwa Kanda ya Kusini.

Kwa upende wake, Mbunge wa Bukoba Mjini, Steven Byabato na Patrobas Katambi wa Shinyanga Mjini, nao walishukuru kwa ujio wa miradi ya TACTIC katika miji yao wakimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongoza mapinduzi makubwa ya kiuchumi na kustawisha Jamii kupitia Miradi ya TACTIC, wenye lengo la kuboresha miundombinu ya miji 45 ya Tanzania pamoja na kujenga uwezo wa Halmashauri ili ziweze kujiimarisha na kutoa huduma zenye ubora kwa wananchi wanaowahudumia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *