
Na Mwandishi WetU, Dodoma
NAIBU wa Waziri wa Nishati, Judith Kapinga, amesema kuwa kuweka mifumo ya kidijitali inaweka uwazi na uwajibikaji katika utoaji wa huduma na kuchochea kukua kwa uchumi.
Kapinga aliyasema hayo wakati alipomwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri Nishati Dkt. Doto Biteko wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Uwekezaji TANESCO (TIMS) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema kuwa TANESCO kuzindua mfumo huo ni moja ya mikakati ya Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka mifumo ya serikali kusomana pamoja na mifumo mingine inayokwenda kuondoa usumbufu kwa wananchi wanapotaka huduma.
Naibu Waziri Kapinga amesema kuwa kuna ufanisi katika sekta ya nishati kwa kuchangia pato la Taifa asilimia 14.4 kutoka asilimia Tano kwa miaka ya nyuma.
Aidha amesema kuwa mfumo wa TANESCO wa TIMS kutaongeza uwekezaji wa miradi ya umeme nchini kutokana wawekezaji wataingia katika mfumo na watajibiwa katika mfumo huo huo bila ya kufika ofisini na makaratasi.
Hata hivyo amewapongeza TANESCO kwa ubunifu wa mfumo huo uliokwenda kufanywa na watumishi ndani ya Shirika na kufanya Serikali kuokoa fedha katika kutengeneza mfumo huo wa kidijitali.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Lazaro Twange, alisema kuwa mfumo huo utavutia wawekezaji wengi katika miradi ya umeme kutokana kuweka kila kitu ndani ya mfumo.
Alisema kuwa kinachofanyika kwa TANESCO kutekeleza maagizo ya Serikali juu ya kuwa na mifumo ya kidijitali katika kuondoa urasimu katika utoaji wa huduma za uwekezaji.
Aidha amesema kuwa katika mifumo uwazi na uwajibikaji unaonekana na matokeo yake yanakua ya haraka kwenye utekelezaji.
Naibu Mkurugezi wa Mipango na Utafiti wa TANESCO Lenatha Ndege, alisema kuwa wametengeneza mfumo wa kidijitali wa TIMS ili kuendana na kasi ya Serikali kuwa na miradi ya ubia na wawekezaji ambapo maombi yote yatafanyika ndani ya mfumo kwa watu wa ndani na nje ya nchi.
Lenatha alisema mfumo huo umetengenezwa kwa kutumia rasiliamali watu kutoka ndani ya Shirika kwa kufanikisha kwa weledi.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Isaac Chanji, alisema kuwa mfumo huo kukamilika ndio adhima ya bodi katika shirika kwenda kisasa kwa kutumia mifumo ya kidijitali.


