MCHENGERWA AIFAGILIA TARURA, MIJI 11 IKISAINI UTEKELEZAJI MKATABA WA TACTIC

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa, amebainisha kuwa Serikali inatambua jitihada na kazi nzuri inayofanywa na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini “(TARURA), akimsihi Mtendaji Mkuu Mhandisi, Victor Seff na wasaidizi wake kutokatishwa tamaa na baadhi ya watu wa mitandaoni.

Waziri Mchengerwa ameeleza wizara yake, Serikali na Bunge la Tanzania wanatambua kazi nzuri inayofanywa na TARURA katika kutekeleza maagizo, maelekezo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha, amesema serikali inatambua ukubwa wa mahitaji na ufinyu wa bajeti unaoikabili TARURA.

“Nipongeze jitihada na kazi kubwa inayofanywa na TARURA kuanzia kwa Mtendaji Mkuu wa TARURA na timu yako, ninawaamini sana, fanyeni kazi wala msirudi nyuma hata kidogo, Bunge na hata wananchi wanajua kazi yenu kwa hiyo msikate tamaa, msikatishwe tamaa na yeyote na wale wanaoandika andika huko, kazi yenu sisi Serikali tunaijua, endeleeni kufanya kazi, kama mngekuwa na bajeti ya kutosha kila Mtanzania angekuwa na furaha lakini Taifa letu ni Taifa changa na kila eneo kuna uhitaji, lakini Taifa letu pia ni kubwa na kila sehemu kuna uhitaji.” Amesema Waziri Mchengerwa.

Wakati wa utiaji saini Mikataba ya utekelezaji wa miradi ya uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania TACTIC, leo Juni 25, 2025 Mjini Dodoma kwa Miji ya Morogoro, Songea, Tanga, Korogwe, Babati, Shinyanga, Bukoba, Bariadi, Lindi, Iringa na Njombe, Waziri Mchengerwa ameonya tabia ya kuchepusha fedha za miradi kunakofanywa na baadhi ya Wakandarasi, naapa kutengua mikataba ya wakandarasi wa namna hiyo katika utekelezaji wa miradi ya TACTIC inayotekelezwa kwenye miji 45 ya Tanzania bara.

“Tunakusudia kuhakikisha kwamba utekeleza wa miradi hii unafanywa kwa wakati. Hatuna changamoto ya fedha kwahiyo sitegemei kuona Mkandarasi analegalega, baadhi ya wakandarasi wakilipwa fedha wanachukua fedha hizo wanapeleka kwenye miradi mingine. Hili sitakubali hata kidogo, iwapo mtaona kuna kulegalega kwa miradi hii tupeni taarifa ili tuweze kufuatilia,” alisema.

Akitaja manufaa ya miradi hiyo, Waziri Mchengerwa alibainisha kuwa miradi ya TACTIC inaenda kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji kote nchini, kuimarisha huduma ya mauzo na manunuzi pamoja na kuongeza thamani ya biashara nchini kwa kuboresha mazingira ya ufanyaji wa biashara kwenye Ngazi ya Miji na Majiji nchini.

Miradi ya TACTIC iliyosainiwa leo ni ya miji 11 ya Tanzania bara, ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa Miradi ya TACTIC kwenye miji 45 ambayo imekuwa ikinufaika na ujenzi wa barabara za viwango vya lami, taa za barabarani, mifereji ya maji ya mvua, ujenzi wa vituo vya mabasi na daladala, ujenzi wa masoko ya bidhaa na mazao mbalimbali, Bustani za mapumziko pamoja na Vivuko vya maji, miradi yote hii ikihusisha takribani Dola za Marekani milioni 410, bila ya kodi ya ongezeko la thamani VAT, ikiwa ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *