Na Daniel Mbega
KATIKA maisha kuna kushinda na kushindwa. Lakini ni muhimu kutambua kuwa ushindi una gharama. Siku zote, lazima mwanadamu jiandae na gharama ya ushindi. Maana, ushindi waweza kuwa ghali mno.
Ndiyo. Unaweza kupambana ukashinda, lakini, gharama ya ushindi yaweza kuwa jamaa na marafiki wa wote uliowashinda watageuka kuwa maadui zako. Yawezekana watakuwa maadui kwako kwa muda mrefu tu. Watakukasirikia, watafanya yote wakiombea nawe upate maumivu.
Lililo muhimu sana ni kwamba lazima ‘Uchague Vita Vyako’! Ni muhimu kujua unapigania nini, wapi, lini na kwa namna gani!
Ili ushinde vita yoyote ni lazima uwe na mikakati imara na thabiti, jeshi imara na lenye nidhamu, mbinu bora, nguvu na mambo mengine kadha wa kadha.
Na tukumbuke tu kwamba, kuanzisha vita si kazi rahisi. Tena inakuwa ngumu zaidi wakati mnapokuwa kwenye uwanja wa mapambano kwa sababu wakati mwingine mbinu za awali inabidi zibadilike kuendana na hali halisi ya uwanja wa mapambano, hasa kwa kuangalia adui anakuja namna gani.
Ndugu zangu, kila mtawala anapoingia madarakani ni lazima apange vipaumbele vyake. Na vingi kati ya vipaumbele hivi huwa ‘ni vita’, kwamba Serikali huelekeza nguvu za mapambano kuhakikisha ushindi unapatikana.
Marais wote waliotangulia walikuwa na ‘vita vyao’. Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na ‘vita vingi’ zaidi kwa sababu ndiyo kwanza tulikuwa tunapata uhuru.
Na katika vita hivyo wapo waliogeuka kuwa maadui wa Mwalimu Nyerere, uadui ambao ulidumu hadi mauti, ingawa alichokipigania ni maslahi ya Watanzania wote.
Vita dhidi ya umaskini, ujinga na maladhi ilianzishwa na Mwalimu na hata sasa bado inaendelea. Mfumo wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea uliofuatia kuzaliwa kwa Azimio la Arusha uliozaa Vijiji vya Ujamaa ulipingwa na wengi, lakini ulikuwa na manufaa makubwa kwa kuwakusanya watu pamoja ili kuwapatia huduma za kiutu.
Walioipinga siasa ile walimchukia Mwalimu. Wengi walitaka ubepari ili kujilimbikizia mali na wakaona mawazo ya Mwalimu yalikuwa yanawachelewesha.
Alhaj Ali Hassan Mwinyi katika awamu yake alikuwa na vita ya ‘Kuufufua Uchumi’, na ndipo tukashuhudia ujio wa ‘Soko Huria’, ujio ambao ndio uliompatia jina maarufu la ‘Mzee Ruksa’.
Mzee Benjamin Mkapa naye alikuwa na ‘Vita ya Rushwa’ na ‘Kudhibiti Uchumi’ baada ya kuonekana hali ilikuwa imeyumba kiasi kwamba fedha zilikuwa mikononi mwa wananchi badala ya Serikali.
‘Mzee wa Msoga’, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, yeye vita yake ilikuwa ‘Dhidi ya Ufisadi’ na mambo mengine kadha wa kadha. Ni katika kipindi chake ambapo tulishuhudia kesi kubwa kubwa za rushwa na ufisadi zikifunguliwa mahakamani.
Tunafahamu kwamba katika awamu ya nne ndipo tulishuhudia vuguvugu kubwa la mabadiliko, siyo tu kutoka kwa wapinzani, bali hata kwa wananchi ambao walikuwa wamechoshwa na vitendo vya rushwa na ufisadi.
Tunafahamu kwamba, vita hivi vilileta uadui mkubwa hata kwa wananchi wenyewe ambao walikuwa wamegawanyika.
Awamu ya tano chini ya Dkt. John Magufuli nayo ilikuwa na ‘vita vyake’ hasa katika kukomesha rushwa na ufisadi, kuhimiza uwajibikaji na kutengeneza uchumi wa viwanda.
Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo kwanza ana mwaka wa pili tangu aingie madarakani Machi 19, 2021.
Lakini tayari tumeona mapambano anayoyaendesha katika kuwaletea Watanzania maendeleo.
Katika kipindi hiki tumeshuhudia jinsi haki za wanawake na watoto, usawa wa kijinsi, masuala ya afya na elimu yakipewa kipaumbele kikubwa.
Wanawake wengi wameteuliwa katika nafasi mbalimbali za uongozi, zikiwemo sekta nyeti ambazo tangu Uhuru tumekuwa tukishuhudia zikishikwa na wanaume pekee.
Tumeshuhudia suala la afya likipewa kipaumbele huku Serikali ikiendelea na mchakato wa Bima ya Afya kwa Watanzania wote.
Suala la elimu haliko nyuma. Mama Samia aliondoa uvumi ulioenea kwamba eti michango na ada vingerejeshwa shuleni. Akasisitiza kwamba elimu itaendelea kutolewa bure, huku akiwaondolea mzigo wazazi kwa uamuzi wa kujenga madarasa 15,000 kwenye shule za msingi na sekondari nchi nzima.
Mama Samia akaenda mbali zaidi katika suala la elimu bila malipo ambapo amefuta ada kwa Kidato cha Tano hadi cha Sita. Sasa watoto wanasma bure kuanzia Elimu ya Awali hadi Kidato cha Sita, achilia mbali mikopo inayotolewa kwa wadahiliwa wa vyuo vikuu.
Nimesoma mara nyingi sana sura zote 13 (mbinu 13 za kivita) za Mwongozo wa mwanafalsafa wa China ya Kale, jenerali wa jeshi, mwandishi na bingwa wa mikakati ya kijeshi, Sun Tzu Wu (inatamkwa Sunzi Wu).
Sun Tzu aliyeishi katika China ya Kale kipindi cha Zhou ya Mashariki (Eastern Zhou) yapata Karne ya 5 Kabla ya Kuzaliwa Kristo, Mwongozo wake wa Sanaa ya Vita (The Art of War), ni makini sana katika mikakati ya kijeshi ambayo dhahiri ndiyo iliyochochea falsafa na tafakuri za kijeshi kwa mataifa ya Magharibi na Asia Mashariki.
Sunzi anasema, unapotangaza vita lazima uzingatie mambo 13: Kuweka mipango; Kupanga vita; Kushambulia kimkakati; Mbinu za kitabia; Nishati au nguvu; Sehemu dhaifu na zenye nguvu; Ujanja; Kutofautisha mbinu; Jeshi kwenye mwendo; Mandhari; Hali tisa; Kushambulia kwa silaha za moto; na Kutumia majasusi.
Mama Samia, kama wale waliomtangulia, ‘alichagua vita vyake’.
Najua vipo vile nilivyovitaja ambavyo alivianzisha, lakini ni dhahiri vipo vingine ambavyo ‘anaviandaa’ ili kuwaletea wananchi maendeleo.
Na vita vyote, ili vifanikiwe kwa faida ya wengi, lazima viache makovu sehemu fulani. Ukitaka kujenga lazima ubomoe! Kwahiyo kuna gharama ya vita.
Wachache wanaojeruhiwa katika vita hivyo hujenga uadui bila kutafakari faida ya wengi iliyopatikana.
Barabara inapojengwa shurti miti na nyumba zivunjwe kuipisha. Na inapojengwa, hurahisisha maendeleo. Barabara inapitisha watu wengi, hata malaika pia!
Kwa maana hiyo, vita yoyote haipiganwi kumfurahisha mmoja, bali hulenga ushindi wa pamoja.
Mwanadamu unapaswa kufikiria gharama ya ushindi wa vita, pamoja na gharama ya kushindwa ikiwa itashindikana. Na wakati mwingine, ni gharama inayostahili kulipwa.
Franklin Roosevelt, Rais wa 32 wa Marekani, alifahamu faida na hasara za kuwa na maadui, hasa katika kipindi kile kigumu cha Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Waliompinga katika sera zake za kiuchumi aliwaita ‘Watiifu wa Kiuchumi’. Na akasema; wamejiunga kwa pamoja kunichukia na nakaribisha chuki zao kwangu!
Kama unapigana vita ya muhimu, na kama vita hivyo vyaweza vikawa vya kushinda (winnable), na kwamba umejiandaa kulipa gharama ya chuki ya muda mrefu ya utakaowashinda, basi, ingia vitani. Ikiwa una mashaka, basi, tafuta suluhu, au rudisha majeshi nyuma kimpangilio (tactical retreat).
Vita vya Mama Samia katika kuwaletea wananchi maendeleo vina umuhimu mkubwa hasa katika kipindi hiki ambacho tayari Tanzania imeingia kwenye Uchumi wa Kati hata kabla ya mwaka 2025!
Vita hivi vya Rais Samia kamwe havitakuwa sawa na vile vya Mfalme Pyrrhic wa Epirus kule Ugiriki ya Kale aliyeamua kuingia vitani kulikabili jeshi kubwa na lenye nguvu nyingi la Warumi.
Rais Samia ana washauri wazuri na ‘anashaurika’, siyo kama Pyrrhic aliyepuuza ushauri wa msaidizi wake wa karibu, Cineas.
Cineas alimuuliza Mfalme; “E bwana Mfalme, Warumi wanasadikika kuwa na jeshi kubwa, lenye nguvu na lenye mashujaa wengi. Ndiyo maana wameteka nchi nyingi. Je, Mungu akitusaidia, tukaja kuwashinda Warumi, tutafanya nini na ushindi wetu?”
Mfalme akajibu: “Mbona hilo ni swali jepesi sana. Mara ile tukiwashinda Warumi, hakutatokea jeshi kutoka mji wowote wa Italia litakaloweza kupambana nasi.”
Cineas akamwuliza tena Mfalme: “Tukishaikamata Italia ya Warumi, kipi kitafuatia?”
Mfalme akajibu: “Sicily ni kisiwa chenye hazina za thamani kubwa, itakuwa rahisi sana kukiteka kisiwa hicho.”
Cineas aliendelea kuuliza: “Bwana Mfalme, unaongea juu ya mambo ya kusadikika, lakini una maana kukitwaa kisiwa cha Sicily kutakuwa na maana ya kukoma kwa vita?”
Mfalme akajibu: “Hapo tutakuwa tumeikaribia Afrika. Na tukishaikamata Afrika ni nani hapa duniani atathubutu kutukabili kivita?”
“Hakuna” Alijibu Cineas, kisha akauliza; “Na baada ya hapo tutafanya nini?”
Mpaka hapo Mfalme hakujua Cineas alikuwa anampeleka wapi kwa lojiki ya kifikra. Mfalme akajibu: “Baada ya hapo, tutapumzika, tutakula raha. Tutakula na kunywa. Tutabaki tukichekeshana na kucheka, siku nzima.”
“Kama ni hivyo,” alisema Cineas; “Ni kitu gani kinachotuzuia kufanya hayo yote sasa bila kwenda vitani?”
Mfalme hakuielewa mantiki ya Cineas. Akakaidi ushauri. Akavipeleka vikosi vyake kupambana na Warumi. Akashinda, lakini akapata hasara kubwa.
Mama Samia anashaurika na vita atakavyovianzisha vitashinda kwa sababu ‘askari’ tuko tayari kumsaidia.
Naam, Mama Samia amechagua vita vyake na ATASHINDA!…
0629-299688