Mwongozo wa uzalishaji mazao kikanda ndiyo dira kwa wakulima

Na Immaculate Makilika – MAELEZO

SEKTA ya Kilimo ni mhimili wa uchumi wa Tanzania na imekuwa ikichangia pato la mkulima mmoja mmoja, kaya na Taifa kwa ujumla pia ni tegemeo la mapato ya fedha za ndani na za nje ya nchi. Sekta hii imeajiri zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu wote nchini na kuzalisha mazao ya chakula na biashara.

Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uzalishaji Mazao kulingana na Kanda za Kilimo za Kiikolojia uliotolewa na Wizara ya Kilimo Juni 2017 wenye lengo la kuzalisha mazao kwa tija na gharama nafuu unaeleza kuwa Tanzania ina Kanda Kuu Saba za Kilimo za Kiikolojia zenye kuwezesha uzalishaji wa mazao ya aina mbalimbali. Kanda hizo ni Kanda ya Kati, Ziwa, Kaskazini, Mashariki, Magharibi, Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kusini.

Mwongozo huo unaoainisha mazao ya kipaumbele kwa kila eneo umeandaliwa ili kuelekeza wawekezaji na wakulima kuchagua zao linaloweza kuzalishwa kwa tija kwa kulingana na hali ya kiikolojia husika.

Aidha, mwongozo umezingatia matokeo ya tafiti zilizofanyika nchini kuhusu aina za udongo, hali ya hewa, mtawanyiko wa mvua na aina za mazao yanayofaa kuzalishwa katika kila eneo.

Hivi karibuni akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alisema kuwa Serikali ilianzisha kanda saba za kilimo na uzalishaji (Tanzania Agriculture Growth Corridors) kwa kushirikiana na Mpango wa Kukuza Kilimo Ukanda wa Kusini (SAGCOT) na imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kilimo katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini kwa kuzingatia ikolojia ya kilimo ya mazao husika.

“Utekelezaji wa miradi katika kipindi chote kwenye ukanda huo ulijikita kwenye kuimarisha tija katika mnyororo wa thamani. Jitihada hizi zimesaidia kuimarisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima, kuongeza matumizi ya teknolojia na upatikanaji wa mitaji,” anaeleza Waziri Bashe.

Waziri Bashe anafafanua: “SAGCOT imewezesha matumizi ya teknolojia bora za kilimo kwenye eneo la hekta 284,098, wakulima 782,452 wameajiriwa katika mnyororo wa thamani wa mazao mbalimbali na kuongeza kipato kwa wakulima cha dola za Marekani milioni 137.”

Aidha, kutokana na uzoefu uliopatikana katika utekelezaji wa Southern Agriculture Growth Corridor of Tanzania – SAGCOT), Wizara imepanga kuanzisha Kanda nyingine saba za uzalishaji (Tanzania Agriculture Growth Corridors) nchini ili kuongeza uzalishaji na tija, kuimarisha masoko ya mazao ndani na nje ya nchi, kuongeza thamani mazao na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo za kilimo, mitaji na kuondoa utamaduni wa kutawanya mazao kila kona ya nchi bila kuzingatia msingi imara wa kibiashara.

Ni dhahiri kuwa Mwongozo wa Uzalishaji Mazao kulingana na Kanda za Kilimo za Kiikolojia ni fursa kwa wakulima na wadau wengine kubaini teknolojia zinazoweza kutumika kwa gharama nafuu bila kuingia gharama katika uzalishaji mazao nje ya ikolojia yake kwa kuboresha mazingira ya asili kama vile kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone na green house ili kukidhi mahitaji ya zao na soko.

Kwa kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za kukuza Sekta ya Kilimo nchini, hivyo basi  mwongozo huu ambao umezingatia malengo ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II)  ukitumika sambamba na miongozo na maelekezo mengine kama vile uzingatiaji wa kanuni za kilimo bora, utawavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kulingana na zao husika.

Mhandisi wa Kilimo Mkoa wa Mara, Okasha Mwita, anasema kuwa Mwongozo wa Uzalishaji Mazao kulingana na Kanda za Kilimo za Kiikolojia ni dira kwa Serikali, wakulima, wafanyabiashara ya mbolea na wadau wote wa Sekta ya Kilimo kwa kuwa unaeleza wakati wa kupanda, kupalilia, kuvuna na aina ya mazao katika eneo husika kulingana na ikolojia.

“Mfano katika mkoa wa Mara, Wilaya ya Serengeti zao la tumbaku linastawi zaidi lakini katika kipindi ambacho ikolojia haiko sawa wakulima wanalima mazao mengine ya biashara na hivyo kuwa na tija katika kufanya shughuli zao za kilimo,” anaeleza Mhandisi Mwita.

Akifafanua zaidi anasema: “Katika Wilaya ya Tarime wakulima wamelima mahindi kwa wingi na kupata mazao mengi kutokana na uwepo wa mvua za kutosha, kuliko wale waliolima katika nyanda za juu. Na kuwa kuwa hakuna mwongozo mwengine zaidi ya huu kwa sasa ni wazi kuwa wakulima wanaolima kwa kufuata mwongozo huu wanalima kwa tija na kwa gharama nafuu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *