Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
IJUMAA, Juni 14, 2024, mtambo namba nane wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), kwa mara ya kwanza umeingiza Megawati 235 zingine kwenye Gridi ya Taifa.
Hatua hiyo inafanya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 2,115 za umeme, kuwa na jumla ya Megawati 470 zinazotumika katika Gridi ya Taifa na kufanya nchi kuwa na ziada ya Megawati 70 baada ya kipindi kirefu.
Akiwa jijini Dodoma, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akizindua Taarifa za Utendaji katika Sekta Ndogo ya Umeme, Gesi Asilia na Mafuta kwa Mwaka 2022/2023, alitangaza hatua ya mtambo namba nane wa JNHPP kuanza kuingiza umeme kwenye Gridi ya Taifa.
Akasema, kwa sasa Megawati 470 zinazalishwa kutoka JNHPP na tayari zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa. Mnamo Februari 2024, Dkt. Biteko alitangaza mtambo namba tisa wa JNHPP kuanza kutoa Megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa, ambazo kwa namna ya pekee zilififisha makali ya mgawo wa umeme ulioanza tangu mwaka 2023, huku akisema upungufu ulikuwa Megawati 200 hadi 400.
Lakini hatua ya mtambo namba nane kuanza kutoa Megawati 235 na hivyo kufanya jumla ya Megawati 470 kutoka JNHPP, imesababisha Taifa sasa kuwa na ziada ya Megawati 70, ziada ambayo ni takriban sawa na uzalishaji wote wa Bwawa la Kufua Umeme la Mtera lililojengwa kati ya mwaka 1970 na 1988, likiwa na mitambo miwili yenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 80.
Hizi ni jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye kwa hakika amevuka malengo na makisio yaliyowekwa na taasisi za kimataifa, ikiwemo Benki ya Dunia.
Uwekezaji mkubwa katika sekta ya nishati unaofanywa na Rais Samia umeleta matokeo ya haraka zaidi, kwani wakati anaingia madarakani Machi 19, 2021 alikuta utekelezaji wa mradi wa JNHPP ukiwa asilimia 37.
Lakini hadi Aprili 2024, utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 97.43 na ukaanza uzalishaji kupitia mtambo namba tisa unaoingiza katika Gridi ya Taifa jumla ya MW 235 na hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme.
Mpaka kufikia hatua hiyo, Serikali imetumia Shs. trilioni 6.01 na kwa mujibu wa taarifa, hivi sasa kazi inaendelea ili kukamilisha ufungaji wa mitambo saba yenye uwezo wa kuzalisha MW 235 kila mmoja.
Utabiri wa Benki ya Dunia
Itakumbukwa kwamba, mnamo Jumatano, Oktoba 31, 2012, Benki ya Dunia ilichapisha utafiti wa wataalamu wake ukionyesha jinsi Tanzania ilivyokuwa ikijikongoja katika huduma ya umeme wa uhakika, ambapo kwa wakati huo ni 14% ya Watanzania waliokuwa wanapata nishati hiyo.
Wataalamu hao, Isis Gaddis, Jacques Morisset na Waly Wane, walieleza katika andiko lao wakionyesha jinsi ukosefu wa huduma ya umeme ulivyokuwa unakwamisha maendeleo ya uchumi.
“Nishati huchochea maendeleo ya uchumi na ushahidi unaonekana machoni mwetu kila siku. Biashara zinahitaji umeme wa uhakika ili kuzalisha bidhaa na huduma. Umeme unawapa fursa watoto kujisomea usiku na hospitali zinahitaji umeme kuokoa maisha yetu,” walisema katika andiko lao.
Wakaongeza: “Uhaba wa huduma ya nishati unahusiana na gharama kubwa za kiuchumi kwa biashara na matumizi ya kaya. Ukosefu wa nishati safi pia huleteleza majanga ya kiafya na kimazingira, kama uchafuzi wa ndani wa mazingira kutokana na mapishi ya kutumia kuni na uharibifu wa misitu kwa ajili ya kupata mkaa na kuni.
“Kwa bahati mbaya, upatikanaji wa nishati safi ni ndoto kwa Watanzania walio wengi, hususan wale wanaoishi pembezoni ya miji na walio maskini: Ni 14% tu ya Watanzania ambao hadi kufikia mwaka 2010 walikuwa wanapata huduma ya umeme.
“Kwa muongo mmoja uliopita (yaani miaka 10 nyuma kabla ya utafiti wao huo), Tanzania imeongeza upatikanaji wa umeme kwa kasi ya 0.1% kwa mwaka. Kwa kiwango hiki, itawachukua hadi karne ya 22 kuweza kufikia malengo ya umeme kwa wote.”
Jitihada za Samia
Lakini Rais Samia ameithibitishia Benki ya Dunia kuwa utabiri wao huo haukuwa sahihi iliposema Tanzania ingeweza kufikia asilimia 100% ya uunganishaji umeme baada ya karne nzima, yaani mwaka 2100, kwani sasa amefanikiwa kufikia malengo hayo miaka 75 kabla ya muda ambao wakubwa hao wa Dunia waliusema.
Hii ni kutokana na kiongozi huyo kwenda na kasi kubwa ya kuunganisha umeme, hasa vijijini, ambapo hadi kufikia Juni 30, 2024 vijiji 4,071 vilivyosalia kati ya vijiji vyote 12,318 vitakuwa vimeunganishwa na nishati hiyo.
Hatua hiyo inafuatia uamuzi wa serikali yake kutoa takribn Shs. trlioni 2.39 katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake ili kutekeleza miradi ya usambazaji umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kiasi cha fedha ambazo Serikali ya Samia imekitoa kimeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini na kuchochea maendeleo na ukuaji uchumi kwa wananchi wa vijijini na kuboresha huduma za kijamii, huku gharama ya kuunganisha umeme ikiendelea kuwa Shs. 27,000 kwa maeneo mengi vijijini.
Licha ya kuwepo kwa janga la Uviko-19, lakini Rais Samia ameendelea kutekeleza miradi ya Umeme Vijiji iliyoachwa na mtangulizi wake kwa kasi ya ajabu, hali ambayo imerahisisha maisha ya wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uunganishaji huu wa umeme vijijini ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Upanuzi wa Umeme Vijijini (TREEP) ulioidhinishwa mwaka 2016, unafadhiliwa kwa pamoja na serikali ya Tanzania, Jumuiya ya Maendeleo ya Kimataifa (IDA), na Mpango wa Kuongeza Nishati Jadidifu (SREP) katika Nchi za Kipato cha Chini za Mfuko wa Mkakati wa Hali ya Hewa (SCF), na kutekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wizara ya Nishati.
TREEP imeundwa kama Mpango wa Matokeo (Programme-for-Result au PforR), unaosaidia Mpango wa Kitaifa wa Umeme Vijijini wa serikali (NREP) kwa kuunganisha kwa njia ya kiubunifu utoaji wa fedha moja kwa moja na utoaji wa matokeo yaliyobainishwa na kufikia malengo yake.
Program ya Matokeo (Program-for-Results – PforR) inalenga kuhudumia maeneo matatu ya uunganishaji kama yalivyobainishwa na NREP: kupanua wigo wa gridi; uunganishaji wa umeme nje ya gridi; na ndani ya malengo ya uunganishaji nje ya gridi, teknolojia za nishati mbadala, ikiwemo umemejua au Jumeme (solar photovoltaic – PV).
Program hiyo ni ya kimkakati na inaakisi Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.
Katika taarifa ya Juni 2022, Benki ya Dunia ilieleza kwamba, katika muongo uliopita, upatikanaji wa umeme nchini Tanzania uliongezeka kutoka asilimia 7 mwaka 2011 hadi 37.7% mwaka 2020, mojawapo ya viwango bora na ongezeko la kasi zaidi katika Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
WB ikasema, ongezeko hilo la kasi la uunganishaji umeme limechangiwa na mambo kadhaa, ikiwa ni pamoja na dhamira kubwa ya kisiasa na uungaji mkono kwa programu za upanuzi wa usambazaji wa umeme vijijini, kuanzishwa kwa ushuru wa petroli kufadhili NREP; na kupunguzwa kwa ada za uunganishaji na gharama za huduma ambazo zilianzishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2013.
Taarifa hiyo ikasema kwamba, pamoja na maendeleo hayo, bado kulikuwa na pengo kubwa kati ya viwango vya upatikanaji wa umeme katika maeneo ya mijini (73.2%) na vijijini (24.5%), na kati ya mtandao wa gridi (78.4%) na kiwango cha jumla cha upatikanaji au uunganishaji (37.7%).
Lakini Benki ya Dunia ikakiri kwamba, Serikali ya Tanzania imedhamiria kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za kisasa za nishati na imejiwekea malengo ya kufikia huduma ya nishati ya kisasa kwa wote ifikapo mwaka 2030, ambapo asilimia 75 itafikiwa na umeme kupitia gridi ya taifa na gridi-ndogo na iliyobaki 25% kupitia uhakiki wa ubora na hasa nishati mbadala.
Hata hivyo, Tanzania iko mbele ya makadirio hayo ya Benki ya Dunia kwa miaka 75 kuhusu usambazaji wa umeme, ikiwa inashika nafasi ya kwanza Afrika kwa kusambaza kwa wastani wa 85% na kuipiga kumbo Nigeria.
Mwaka 2012 Benki ya Dunia ilikadiria kuwa agenda ya kusambaza umeme kwa wote, ingeweza kufikia 100% duniani kote ifikapo karne ya 22 (yaani mwaka 2101), huku Tanzania ikipewa nafasi finyu ya kufikia malengo hayo.
Jitihada za Rais Samia zinadhihirisha bayana kwamba, Tanzania inaweza kuifikia 100% hata kabla ya mwaka 2025, huku program ya REA ikitarajiwa kukamilika Juni 2021 ambapo vijiji vyote Tanzania Bara vitakuwa vimeunganishwa.
Awali, Nigeria ndiyo iliyokuwa inaongoza Afrika kwa 72%, lakini kwa sasa Tanzania iko juu.
Uunganishaji huo wa vijijini-mijini, kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2019/20 unaonyesha kwamba, takriban 99.5% ya wakazi wa mijini wanapata huduma ya umeme wakati kwa upande wa vijijini, wanaopata umeme wamefikia 69.8%, idadi ambayo itakuwa imeongezeka sasa kutokana na ongezeko la vijijini vingi.
Taarifa zinaonyesha kwamba, hadi wakati huo, Mkoa wa Dar es Salaam ndio ulikuwa unaongoza kwa wakazi wake kupata umeme kwa 100%, ukifuatiwa na Kilimanjaro (93.6%), Mwanza (89.9%), Mbeya (89.0%), Mara (87.7%), Pwani (85.8%), Arusha (84.5%), Geita (84.4%), Tanga (83.5%), Kagera (81.8%), Iringa (81.4%), Njombe (80.0%), Tabora (76.4%), Morogoro (74.6%), na Dodoma (74.4%).
Mikoa mitano ambayo usambazaji umeme ulikuwa chini ni Kigoma (56.3%), Manyara (58.1%), Shinyanga (61.7%), Songwe (61.9%) na Rukwa (64.8%), ambayo kwa sasa imepanda pia.
Kasi ya REA
Aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Jones Olotu, alisema Rais Dkt. Samia ni shujaa wa mafanikio makubwa ambayo REA imeyapata kupitia majukumu waliyonayo ya usambazaji nishati ya umeme vijijini katika mikoa mbalimbali Tanzania Bara.
“Kuna miradi mingi ya usambazaji umeme vijijini ambayo inaendelea kutekelezwa, ifikapo Juni mwaka 2024, vijiji vyote Tanzania Bara vitakuwa na umeme na ifikapo 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme,” alisema wakati alipokutana na wahariri jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwaka 2023.
Akasema, umeme unaosambazwa vijijini utasaidia kuhamasisha shughuli za uzalishaji, uanzishwaji viwanda vidogo, vya kati, biashara ili kuchochea uchumi wa vijiji.
Olotu alifafanua kuwa, walengwa wa miradi ya REA ni wananchi waishio vijijini ambao ni asilimia 75 ya wananchi wote Tanzania Bara wanaofikia 59,851,347.
Miradi inayotekelezwa na REA ni kuongeza wigo wa Gridi ya Taifa katika vijiji, vitongoji vyote nchini ili kufikisha huduma kwa wananchi wengi vijijini.
Pia kuna miradi ya nje ya gridi inayojumuisha mifumo midogo ya kuzalisha na kusambaza umeme katika maeneo yenye vyanzo vya nishati Jadidifu.
Anafafanua miradi hiyo kuwa ni pamoja na kufunga mifumo ya umeme jua katika taasisi za serikali, maeneo ya huduma za jamii yaliyopo vijijini.
Pia kusambaza nishati safi na salama ya kupitia, REA imewezesha ujenzi wa mitambo ya hewakani (biogass) majumbani, kwenye taasisi za elimu, kambi za jeshi, magereza.
Anasema, Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili unahusisha kupeleka umeme kwenye vijiji 4,071 vilivyobaki kati ya vijiji vyote 12,318.
Pia kujenga njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 23,526, kujenga njia za umeme wa msongo mdogo urefu wa kilomita 12,159, kufunga mashineumba (transformer) 4,071, kuunganisha wateja wa awali wapatao 258,660.
Mradi huo unafadhiliwa na serikali ya Tanzania ikishirikiana na Benki ya Dunia kwa gharama ya Shs. trilioni 1.58, unatarajiwa kukamilika Desemba 2023.
Mhandisi Olotu akasema, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa kufikisha umeme katika vitongoji (Hamlet Electrification Project – HEP) ili kuhakikisha kuwa umeme unatumika maeneo yote ya vijijini Tanzania Bara.
Serikali kupitia REA ilifanya utambuzi wa wigo wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji vyote Tanzania Bara na kubaini kuwa vitongoji ambavyo bado havijafikiwa na miundombinu ya umeme nchini ni 36,101 kati ya vitongoji 64,760 vilivyopo Tanzania Bara.
Anasema, gharama za kufikisha miundombinu ya umeme katika vitongoji hivyo (36,101) ni Shs. trilioni 6.7.
“Kuna Mradi wa Ujazilizi Mzunguko wa Pili B ambao unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,686 katika mikoa ya Arusha, Geita, Kagera, Katavi, Kigoma, Lindi, Morogoro, Njombe na Songwe na kuunganisha jumla ya wateja wa awali 95,334. Gharama ya mradi huu ni Shs. bilioni 234.4 na unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD),” alisema Olotu.
Kuhusu Mradi wa Ujazilizi Mzunguko wa Pili C, anasema, unalenga kuongeza wigo wa usambazaji umeme kwenye vitongoji 1,880 katika mikoa ya Manyara, Iringa, Rukwa, Mtwara, Ruvuma, Simiyu na Mara kwa kujenga kilomita 6,562 za msongo mdogo na kufunga mashineumba 1,932 ili kuunganisha wateja wa awali 131,719, ambapo gharama yake ni Shs. bilioni 293 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali za Norway na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Mnamo Januari 4, 2024, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, aliwaagiza wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya kusambaza umeme vijijini kukamilisha kazi kwa muda waliopewa kwa mujibu wa mikataba.
“Wanaochelewesha miradi wanawazuia wananchi kupata huduma kwa wakati kwa sababu hiyo hakuna nyongeza ya muda itakayotolewa kwa wakandarasi ambao watachelewa kukamilisha miradi,” alisema Mhandisi Saidy wakati akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili mkoa wa Tanga.
Kwa ujumla, kuna miradi mingi ambayo Serikali ya Samia inaendelea kuitekeleza kwa kasi katika kuhakikisha kwamba uchumi shirikishi na fungamanishi unachochewa na upatikanaji wa nishati ya uhakika.
Anatekeleza Lengo Namba 7
Kasi ya kutekeleza miradi ya umeme vijijini inayofanywa na Serikali ya Rais Samia inakwenda sambamba na Lengo Namba 7 na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs) yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015.
Inaelezwa kwamba, mpaka sasa watu milioni 733 ulimwenguni hawapati huduma ya umeme huku watu bilioni 2.4 wakiendelea kupika kwa kutumia kuni na mkaa na Ripoti ya Benki ya Dunia inasema, kwa kasi ndogo ya sasa ya uunganishaji umeme, watu milioni 670 wanaweza kuwa hawajaunganishwa ifikapo mwaka 2030 kutokana na changamoto ya Uviko-19 iliyotokea.
Bara la Afrika linatajwa kwamba linaendelea kuburuza mkia ambapo watu milioni 568 hawajaunganishwa na nishati ya umeme mpaka sasa, ambapo asilimia 77 kati yao ni kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Lengo Namba 7 la pia linahusu ufanisi wa nishati. Kuanzia mwaka 2010 hadi 2019, maboresho ya kila mwaka ya kiwango cha nishati duniani yalikuwa wastani wa asilimia 1.9. Hii iko chini ya viwango vinavyohitajika ili kufikia malengo ya SDG 7 na ili kufidia hali iliyopotea, kiwango cha wastani cha uboreshaji kingeongezeka hadi asilimia 3.2.
Vipaumbele vikuu vya Lengo Namba 7 ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika, nishati safi ya kupikia, nishati mbadala, na kadhalika.
Haya ndiyo mambo ambayo yanazingatiwa na Serikali ya Awamu ya Sita ambayo inaendelea kupambana usiku na mchana kuhakikisha Tanzania inaunganishwa na nishati ya umeme na kuhimiza wananchi kutumia nishati mbadala, ikiwemo gesi asilia, katika kupikia pamoja na vyombo vya usafiri.