- Yasafirisha korosho tani 230,000, makaa ya mawe tani 600,000 msimu huu
Na Daniel Mbega, Mtwara
BANDARI ya Mtwara imekwishasafirisha takriban tani 230,000 za shehena ya korosho ghafi kwenda nje, ukiw ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyoyatoa miezi minne iliyopita.
Mbali ya shehena hiyo ya korosho, kati ya Julai 2023 na Januari 2024 bandari hiyo pia imesafirisha karibu tani 600,000 za makaa ya mawe ambayo yanachimbwa kutoka Ngaka na Mbamba Bay mkoani Ruvuma.
Ijumaa ya Septemba 15, 2023, wakati alipofanya ziara kwenye Bandari ya Mtwara, Rais Samia aliagiza kwamba, korosho zote za Mikoa ya Kusini zisafirishwe kupitia bandari hiyo badala ya kupelekwa Dar es Salaam.
Katika maagizo hayo, Rais Samia alisema kwamba, yeyote anayetaka kusafirisha kwa bandari nyingine aombe kibali kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, hali ambayo iliashiria kuwa Mtwara sasa imekuwa ‘Bandari ya Korosho’.
“Serikali yangu itaendelea kuongeza bajeti ya kuboresha miundombinu ya Bandari ili kuvutia zaidi wateja, wadau wafanyabiashara wa usafirishaji bidhaa mbalimbali ili kuongeza ushawishi wa kuzitumia zaidi bandari zetu,” alisema Rais Samia.
Akatoa rai kwa watumishi wa Bandari ya Mtwara kufanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa ili Bandari hiyo ifikie kiwango cha Bandari ya Dar es Salaam.
Miradi iliyotekelezwa kama sehemu ya maboresho ya utendaji kazi wa Bandari ya Mtwara ni pamoja na ujenzi wa Gati moja la nyongeza lenye urefu wa mita 300, ujenzi wa mita ya kupimia mafuta ili kuhakikisha mafuta yanayoshushwa katika Bandari ya Mtwara yanapimwa, ujenzi wa sehemu ya kuhifadhi Makasha na ukarabati wa ghala na vifaa vya kuhudumia mizigo bandarini.
Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 TPA kupitia bandari zake zote nchini ilihudumia jumla ya shehena tani milioni 24.899 ambapo Bandari ya Dar es Salaam ni kinara kwa kuhudumia shehena tani milioni 21.461 ikifuatiwa na Bandari ya Mtwara iliyohudumia shehena tani milioni 1.63.
Maagizo ya Rais Samia yanamaanisha kupunguza usafirishaji wa korosho kwa kutumia barabara hadi kwenye Bandari ya Dar es Salaam, hiwa kuwapa unafuu wasafirishaji wa zao hilo.
Mbali ya hilo, maagizo hayo yanaleta tija na thamani halisi ya uwekezaji uliofanywa katika Bandari ya Mtwara, ambapo Serikali iliwekeza zaidi ya Shs. bilioni 47 ili uongeza ufanisi bandarini hapo, uwekezaji ambao umeshuhudia kiwango cha kuhudumia mizigo bandarini hapo kikiongezeka kutoka tani 592,000 hadi tani 1,630,000 kwa mwaka.
Mbali ya ukarabati huo, Serikali pia imeandaa mpango wa kujenga bandari maeneo ya Kisiwa Mgao ambayo inatarajiwa kugharimu Shs. bilioni 150.
Taarifa kutoka bandarini hapo zinaeleza kwamba, mwezi mmoja baada ya agizo hilo la Rais Samia, mnamo Oktoba 2023 Bandari ya Mtwara ilipokea shehena ya makasha zaidi ya 300 kwa ajili ya maandalizi ya usafirishaji wa korosho ghafi.
Kasi kubwa inaendelea
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari waliozuru bandarini hapo mwishoni mwa wiki, Meneja wa Bandari Mtwara, Ferdinand Nyathi, amesema tangu walipoanza utekelezaji wa maagizo hayo meli nyingi zimekuwa zikitia nanga kupakua makasha tupu na kupakia shehena ya makasha ya korosho.
“Ili kuhakikisha tunatekeleza maagizo ya Rais Samia ya korosho zote kusafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara tumejipanga kwenye vifaa na Serikali imeshaleta mitambo mingi mikubwa ambayo tuna imani kuwa italeta ufanisi mkubwa na kusaidia kuharakisha ushushaji na upakiaji wa makasha,” anasema.
“TPA imepokea “crane” ya kisasa iitwayo “Ship to Shore Gantry Crane (SSG)”, mtambo huu umeshasimikwa katika Bandari ya Mtwara na una uwezo wa kuhudumia makasha 25 (TEUs) kwa saa. Pia kuna Scanner moja ambayo inaweza ‘scan’’ hadi makasha 30 kwa saa.
“Bandari ina maghala mawili ya kuhifadhia mizigo (Zambia Shed na Shed No. 3) yenye ukubwa wa mita za mraba 12,500 na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 18,000 za mizigo kwa wakati mmoja,” anaendelea kufafanua Nyathi.
Kicheko kwa wakulima
Hatua ya Bandari ya Mtwara kusafirisha korosho moja kwa moja imewapa tabasamu wakulima pamoja na wadau wengine wa zao la korosho, ambao sasa wanaweza kuokoa gharama za usafirishaji tofauti na ilivyokuwa mwanzo.
Msimu wa 2023/2024 ambao umeanza Oktoba 2023 ndio wa kwanza kushuhudia shehena kubwa ya korosho ikisafirishwa kwenda ng’ambo kupitia bandari hiyo na kwa kuwa korosho ni zao linalolimwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, bandari hiyo ina haki ya kuitwa ‘ya Korosho’.
Mkoa wa Mtwara ndio ulio katikati kwa wakulima na wadau wa korosho wa mikoa hiyo ya kusini ambapo hata wafanyabiashara wanapata “usingizi” mnono kwa vile hawana haja tena ya kukesha kuhakikisha shehena zao kama zimefika salama Dar es Salaam au la baada ya kuhangaika na malori katika vijiji na halmashauri za mikoa hiyo wakati wa kukusanya mzigo.
Mara baada ya “kufunguliwa kwa milango” ya kusafirishia korosho kupitia bandari hiyo makumi kwa mamia ya malori yenye shehena yalikuwa yakifurika bandarini hapo kubeba makasha tupu na kuingiza yaliyojazwa kabla ya taratibu nyingine za usafirishaji.
Uwepo wa vifaa vya kisasa kama crane ya kisasa ya SSG na Scanner ya kisasa unarahisisha uhakiki wa makasha kwa muda mfupi, hivyo kuondoa usumbufu wa kusubiri muda mrefu.
Kwa sasa, Meli ya CMA-CGM Puerto Antioqua imetia nanga bandarini hapo ambapo kwa mujibu wa Meneja wa Bandari Bw. Nyathi, ilikuja na makasha tupu 700 ya urefu wa futi 40 kwa ajili ya kujaza korosho na mpaka sasa imekwishajaza nusu yake.
Hali ya utendaji kazi
Korosho ndiyo shehena inayoibeba Bandari ya Mtwara kwa asilimia 60, ndivyo anavyosema Meneja wa bandari hiyo, Ferdinand Nyathi, ambaye anaongeza pia kwamba shehena nyingine kubwa ni makaa ya mawe.
Akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Nyathi anasema, rekodi zilizopo zinaonyesha kwamba ufanisi bandarini hapo umeongeza kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na miaka 10 nyuma.
Rekodi zinaonyesha kwamba, kabla ya ukarabati mkubwa kufanyika, mwaka 2013/14 Bandari ya Mtwara ilihudumia tani 356,356 kwa ujumla ikiwemo na korosho, lakini mwaka 2014/15 ikashuka kwa kuhudumia tani 296,577 na mwaka uliofuatia 2015/16 idadi ikakashuka tena kufikia tani 268,035 kabla ya kupanda hadi kufikia tani 377,590 mwaka 2016/17.
Ujenzi wa gati mpya yenye urefu wa mita 350 na kina cha mita 13 umesaidia kuhudumia kiasi kikubwa kwani linawezesha meli mbili kubwa na meli moja ya mwambao kutia nanga kwa wakati mmoja, tofauti na gati la zamani ambalo linaweza kuhudumia meli moja tu kubwa.
Tangu wakati maboresho yalipokamilika, utendaji kazi bandarini hapo umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 100 ambapo kwa mwaka 2021/22 walihudumia tani 500,000 lakini mwaka 2022/2023 walihudumia tani milioni 1.63 huku meli zilizohudumiwa zikiongezeka kutoka 166 mwaka 2021/2022 hadi 180 mwaka 2022/23.
Kwa ujumla, Serikali imedhamiria kuhakikisha pato linalokusanywa kupitia bandari linavuka asilimia 50 na utekelezaji wake ulianza kwa kufanya maboresho ya miundombinu na sasa inakwenda na mkakati wa kushirikisha wadau ili kuja na suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazojitokeza.
Akitoa ufafanuzi wa ufanisi na kiasi cha shehena kilichohudumiwa bandarini hapo, Nyathi anasema kwamba, katika kipindi cha mwaka 2018/19 hadi Januari 2024 walipakua na kupakia jumla ya tani 3,794,371 ambapo zilizopakuliwa zilikuwa jumla ya tani 410,948 na zilizopakiwa zilikuwa tani 3,383,423.
Kulingana na takwimu zilizotolewa na Bandari hiyo, shehena iliyopakuliwa kwa mwaka 2018/19 ilikuwa tani 45,072, mwaka 2019/20 (tani 30,433), mwaka 2020/21 (tani 42,225), mwaka 2021/22 (tani 85,887), mwaka 2022/23 (tani 92,190), na kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2024 tani zilizopakuliwa zilikuwa 115,141.
Aidha, tani zilizopakiwa kwa mwaka 2018/19 zilikuwa 61,098, mwaka 2019/20 (243,034), mwaka 2020/21 (135,163), mwaka 2021/22 (506,488), mwaka 2022/23 (1,536,485), na kuanzia Julai 2023 hadi Januari 2024 jumla ya tani 901,155 zimekwishapakiwa.
Kwa upande mwingine, jumla ya meli 1,001 katika kipindi cha mwaka 2018/19 hadi Januari 2024, zikiwemo meli 324 za kimataifa na meli 677 za mwambao.
Takwimu zinaonyesha kuwa, meli za kimataifa zilizohudumiwa mwaka 2018/19 zilikuwa 16, mwaka 2019/20 (32), mwaka 2020/21 (26), mwaka 2021/22 (50), mwaka 2022/23 (106), na kati ya Julai 2023 hadi Januari 2024 meli 94.
Kwa upande wa meli za mwambao, mwaka 2018/19 zilizohudumiwa zilikuwa 125, mwaka 2019/20 (78), mwaka 2020/21 (58), mwaka 2021/22 (116), mwaka 2022/23 (207), na kati ya Julai 2023 hadi Januari 2024 meli 93.
Aidha, jumla ya shehena ya makasha (TEUs) 52,371 yalihudumiwa bandarini hapo yakiwemo 27,651 yaliyopakuliwa na 24,720 yalipakiwa kwenye meli kwenda sehemu mbalimbali.
Ufanisi haukuwa mzuri sana katika kipindi hicho kutokana na uwepo wa janga la Uviko-19 lililoikumba Dunia ambapo katika mwaka 2020/21 na 2021/22 hakuna makasha yaliyopakiwa na katika mwaka 2021/22 hakuna kasha lililoshushwa kwa vile hata idadi ya meli zilipungua.
Bandari hiyo imekuwa muhimu hata kwa nchi jirani ya Msumbiji, hususan kaskazini mwa nchi hiyo, ambako kuna vurugu za wanamgambo wa ISIS, hususan kwenye Jimbo la Nampula.
Ingawa vikosi vya ulinzi wa Amani vya SADC vipo huko, lakini hali ya usalama imeonekana kuwa ya wasiwasi na wawekezaji katika sekta ya gesi wanashindwa kuitumia Bandari ya Nacala kwa kuhofia hujuma, hivyo mbadala pekee unaweza kuwa Bandari ya Mtwara.
Kwa ujumla, maagizo ya Rais Samia ya kuifanya Mtwara kuwa Bandari Maalum ya kusafirishia korosho yamezaa matunda, lakini bandari hiyo itazidi kushamiri endapo wadau wengine, wakiwemo wawekezaji katika sekta ya viwanda na uchimbaji madini, wataamua kwa dhati kuitumia bandari hiyo, hali ambayo itakuza mapato ya Taifa.