Maboresho ya miundombinu yaipaisha Bandari ya Mtwara

Na Daniel Mbega, Mtwara

MIAKA saba iliyopita Bandari ya Mtwara haikuwa na shughuli nyingi za kiuchumi siyo kutokana na kutokuwepo kwa uhitaji, bali kutokana na miundombinu iliyokuwepo ambayo haikukidhi meli kubwa kutia nanga hapo.

Lakini tangu Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ilipodhamiria kuboresha miundombinu kwa kupanua gati ili kuwezesha meli kubwa kutia nanga bandarini hapo.

Maboresho hayo yameipa hadhi kubwa Bandari ya Mtwara ambayo kimkakati ina uwezo wa kuhudumia nchi za jirani za Comoro, Malawi, Msumbiji na Zambia pamoja na Mikoa ya Ukanda wa Kusini mwa Tanzania ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ambayo ina fursa kubwa za kiuchumi, ikiwemo uchimbaji wa madini.

Meneja wa Bandari ya Mtwara, Ferdinand Nyathi, anatoa rai kwa Serikali iendelee kutekeleza mipango yake katika kuboresha miundombinu ya usafirishaji wa nchi kavu hasa reli, ili kuchochea matumizi ya Bandari ya Mtwara kwa kuiunganisha na maeneo mbalimbali ya Ushoroba wa Mtwara.

Tangu mwaka 2016, TPA ilianza mkakati wa kukuza mapato ya Serikali na kuongeza ajira kwa kuboresha miundombinu katika Bandari ya Mtwara na nyingine ndogo za Lindi na Kilwa.

Kuboreshwa kwa miundombinu ya Bandari Mtwara kunachochea fursa nyingi ambazo ni pamoja na kuhudumia bidhaa za viwanda vinavyojengwa mkoani Lindi na Mtwara na mazao mblimbali yapatikanayo katika mikoa hiyo, hasa korosho.

Maboresho katika bandari hiyo, kwa mujibu wa Nyathi, ni pamoja na kuikarabati gati ya awali ambayo ina urefu wa meta 120 lakini gati mpya ambayo ukuta wake una urefu wa meta 385 na inawezesha meli nne kutia nanga na chombo kimoja cha mwambao kwa wakati mmoja.

“Bandari hii ina kina cha meta 9.5 hadi 13.5 huku ikiwa na vifaa vya kisasa vya kuongozea meli vinavyotumia umeme wa jua, meli zinaweza kuingia bandarini muda wowote katika saa 24 za siku. Hapa hakuna masharti ya maji kupwa na maji kujaa kwa meli zinazoingia na kutoka bandarini,” anasema Nyathi.

Nyathi anaongeza kwamba, maboresho yaliyofanywa ni pamoja na miundombinu ya kuhudumia shehena iliyopo ambapo ni pamoja na zana mbalimbali za kupakilia, kupakulia na kupanga.

Zana hizo ni kreni kubwa ya kupakia na kupakua shehena za makasha kwenye meli (SSG), winchi inayotembea yenye uwezo wa tani 100, Reach Stacker zenye uwezo wa kubeba tani 45 kila moja, Front Loader tani 42, winchi zinazotembea zenye uwezo wa tani 50 na tani 25, mitambo ya kubeba makasha matupu, foko zinazobeba tani 16, tani 5 na tani 3, matrekta, Hoppers na Grabs.

Aidha, anasema, kuna mashua za kusogezea meli na kuongoza (Tug Boat na Mooring Boat).

Maboresho hayo yanahusisha pia maghala makuu mawili ya shehena yenye jumla ya zaidi ya eneo la meta za mraba 15,000. Hifadhi ya wazi iliyojengwa kwa jumla ya meta za mraba 124,000 ikijumuisha meta za mraba 76,000 iliyojengwa mwaka 2020 na hifadhi nyingine ya wazi ya meta za mraba 20,000.

Kutokana na maboresho hayo, uwezo wa sasa wa Bandari ya Mtwara ni kuhudumia tani 1,000,000 za shehena zinazoingizwa na kusafirishwa nje kwa mwaka.

“Kwenye gati la zamani kuna yadi 3 zenye ukubwa wa mita za mraba 38,000 na uwezo wa kuhifadhi makasha 4,350 (TEUs) kwa wakati mmoja. Gati hili za zamani lina kina cha mita 9.5 (Chart Datum – CD), urefu wa mita 385 na uwezo wa kuhudumia hadi tani 45,000DWT.

“Gati jipya lina kina cha mita 13.0 (Chart Datum), urefu wa mita 300 na uwezo wa kuhudumia hadi tani 65,000DWT ambapo ujenzi wake uligharimu Shilingi bilioni 157.8. Gati hili jipya lina yadi yenye ukubwa wa mita za mraba 75,807, uwezo wa kuhifadhi makasha 8,600 TEUs kwa wakati mmoja. Upana wa lango la kuingilia meli ni mita 250 na kina cha zaidi ya mita 20,” anafafanua Nyathi.

Nyathi anaeleza kwamba, Bandari ya Mtwara ina mizani sita (6), ina Kituo cha kupimia mafuta (Flow Meter) inayopima mafuta ili kuweza kujiridhisha kiwango cha mafuta kinachoshuka melini.

Mifumo ya Tehama inatumika bandarini hapo kwani ina mifumo ya Baharini, Mizigo na Malipo kwa ajili ya kushughulikia kila aina ya mizigo.

“TPA imepokea “crane” ya kisasa iitwayo “Ship to Shore Gantry Crane (SSG)”, mtambo huu umeshasimikwa katika Bandari ya Mtwara na una uwezo wa kuhudumia makasha 25 (TEUs) kwa saa. Pia kuna Scanner moja ambayo inaweza ‘scan’’ hadi makasha 30 kwa saa.

“Bandari ina maghala mawili ya kuhifadhia mizigo (Zambia Shed na Shed No. 3) yenye ukubwa wa mita za mraba 12,500 na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 18,000 za mizigo kwa wakati mmoja,” anaendelea kufafanua Nyathi.

Fursa zilizopo

Ukanda wa Kusini una fursa nyingi za uchumi kuanzia kilimo cha mazao mbalimbali yanayozalishwa katika Mkoa wa Mtwara na mikoa ya jirani ya Lindi na Ruvuma ikiwemo ufuta na korosho.

Lakini pia kuna shughuli za utafutaji wa Mafuta na Gesi, uzalishaji wa Gesi Asilia na bidhaa zitokanazo na Gesi.

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi, kuna fursa za ujenzi wa miradi ya miundombinu na viwanda inayotarajiwa katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma, lakini pia uwepo wa bidhaa za madini na viwanda mbalimbali katika Ushoroba wa Maendeleo wa Mtwara (Mtwara Development Corridor) na nchi jirani za Msumbiji, Malawi na Zambia.

Meneja wa Bandari hiyo, Bw. Nyathi, anasema kwamba wanaopitisha bidhaa kwenye bandari hiyo wanaokoa takriban 30% ya gharama ikilinganishwa na bandari nyingine.

“Bandari ya Mtwara hutoza Tozo ya Wharfage kwa 0.5% kwa Mizigo ya Makasha (containerized cargo) inayosafirishwa au kupokewa (Export and Import). Bandari nyingine hutoza Wharfage kwa 1%,” anasema. “TPA imepunguza tozo ya ‘Shore Handling’ na ‘Stevedoring’ kwa asilimia 30 kwa Bandari ya Mtwara ukilinganisha na bandari nyingine ambazo hutoza 100%.”

Anaongeza kwamba, wameongeza muda wa hifadhi ya Makasha matupu (Empty Container) kutoka siku 15 hadi 21 lakini pia wameongeza muda wa hifadhi ya makasha yenye mzigo (Full Containers) kutoka siku 7 hadi 14.

Kutokana na maboresho hayo, hata wawekezaji waliowekeza Ukanda wa Kusini wanayo fursa kubwa ya kuitumia Bandari ya Mtwara kusafirisha mizigo na vifaa vyao mbalimbali kuliko kupitishia Dar es Salaam ambako wanalazimika tena kusafirisha kupitia njia ya barabara.

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas, amewataka wawekezaji hao wa ndani na nje kuitumia bandari hiyo kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa ambayo yanaleta unafuu na kupunguza gharama za uwekezaji.

Kwa sasa bandari hiyo inasafirisha shehena mbalimbali kutoka ndani kwenda nje ikiwemo makaa ya mawe yanayochimbwa mkoani Ruvuma, shehena ya korosho ambayo zamani ilikuwa ikisafirishwa kupitia Bandari ya Dar es Salaam pamoja na madini mbalimbali yakiwemo ya vito.

Meli kubwa zinatia nanga bandari hapo kushusha shehena ya Sulphur ambayo inatumiwa na wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma.

“Kulingana na ripoti za TPA, Bandari hii inapitisha mizigo mingi kwa sababu meli kubwa za shehena zinatia nanga kushusha na kupakia shehena, hivyo ni fursa nzuri kwa wawekezaji kuitumia kwa faida yao na kukuza uchumi wa taifa,” anasema Kanali Abbas.

Lakini Meneja wa Bandari hiyo, Ferdnand Nyathi, anasema ingawa zipo changamoto kadhaa wao wanazichukulia kama fursa.

Hata hivyo, anazidi kuiomba Serikali kuendelea na uboreshaji wa miundombinu kwa sababu ukosefu wa miundombinu ya usafirishaji wa ardhini kama Reli ambayo ingekuwa ni kiunganishi kutoka maeneo ya uzalishaji kama migodini (Mbamba Bay, Mchuchuma na Liganga).

Anasema pia kwamba, ukosefu wa meli za mwambao za uhakika ambazo zingesadia kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka Mtwara kwenda Tanga na Dar es Salaam na nchi jirani ya Comoro ni kikwazo kingine.

Historia ya Bandari

Bandari ya Mtwara ina jumla ya Hekta za mraba 2,712 za wrdhi ambazo zinaweza kutumika kwa upanuzi na uendelezaji wa Bandari wakati wowote.

Nyathi anafafanua kwamba, eneo ilipo Bandari kwa sasa ina ukubwa wa hekta za mraba 70, Kisiwa Mgao kina ukuwa wa hekta za mraba 25, Msangamkuu na Ng’wale kuna ukubwa wa hekta za mraba 2,623 ambako kunaweza kupanuliwa wakati wowote yakitokea mahitaji.

Kijiografia inapatikana kilomita 578 Kusini mwa Jiji la Dar es Salaam.

Kihistoria, Bandari ya Mtwara ni miongoni mwa Bandari kuu tatu (3) za mwambao wa Bahari ya Hindi, zilizo chini ya TPA. Bandari nyingine ni Dar es Salaam naTanga.

Bandari hiyo pia inasimamia Bandari za Lindi na Kilwa.

Bandari ya Mtwara iliimarishwa wakati wa ukoloni na Waingereza mnamo miaka ya 1948-1954, na reli ilijengwa ikiunganisha bandari hiyo, kama sehemu ya Mradi wa Karanga wa Tanganyika huko Nachingwea. Kwa sababu ya kutokufanikiwa kwa mradi huo, ambao ulikuwa pacha na ule wa Kongwa mkoani Dodoma, bandari hiyo ilipoteza thamani yake na reli iliondolewa.

Bandari ya Mtwara inarahusisha shughuli za biashara kwa Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na Zanzibar pamoja na nchi za Msumbiji, Comoro, India na Vietnam na Mashariki ya Kati.

Bidhaa kuu zinazopita Bandari ya Mtwara ni pamoja na korosho ghafi, saruji, bidhaa za chakula, shehena ya miradi, mafuta, makaa ya mawe pamoja na mizigo mchanganyiko.

Bandari hiyo ilikuwa ikifanya kazi lakini haikutumika sana kwa miaka mingi kutokana na miundo mbinu mibovu ya uchukuzi. Lakini, katika miaka ya 2010-2011 kutokana na kuongezeka kwa shughuli katika utaftaji wa rasilimali ya mafuta na gesi, shughuli za bandari ziliongezeka.

Awali Bandari imeshughulikia shehena kidogo sana kutokana na kukosekana kwa viwanda vikubwa katika eneo hilo. Uuzaji mkubwa wa nje ya bandari umekuwa ni zao la korosho kila mara.

Bandari ina ukuta wa mita 385. Hapo awali bandari hiyo ingeweza kupokea meli 2 za urefu hadi mita 175. Tangu ukarabati wa mwaka 2015, bandari hiyo inaweza kushughulika pia meli ya mita 209. Bandari hiyo inashughulikia tani 1,000,000 za mizigo kila mwaka ambazo ni chini ya asilimia 5 (5%) ya jumla za shehena za nchi, hata hivyo.

Bandari pia ina eneo maalum la kiuchumi lililounganishwa na bandari hiyo. Mnamo Desemba mwaka 2015 “Alistair Freeports Limited” iliingiza  dola za Kimarekani 700,000 kuboresha “eneo la usindikaji” karibu na eneo la bandari.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *