Na Mwandishi Wetu, London
WIZARA ya Madini imezinadi leseni 441 za utafutaji madini muhimu na mkakati ambapo kati ya hizo, leseni 46 kwa ajili ya uchimbaji madini hayo hivyo kutoa fursa kwa wawekezaji kuingia ubia na wamiliki wa leseni hizo kuziendeleza na hatimaye kuanzisha migodi.
Kamishna Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Mhandisi Ally Samaje aliyasema hayo wakati akitoa wasilisho la Wizara katika Jukwaa la Biashara.
Jukwaa hilo linafanyika nchini Uingereza likishirikisha nchi hiyo na Tanzania akitumia fursa hiyo kuwaeleza washiriki madini muhimu, mkakati uliopo Tanzania.
Mhandisi Samaje alisema, kati ya leseni hizo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linayo miradi ya utafutaji madini muhimu ya lithium na graphite.
Mengine ni rare earth elements na shaba ambayo iko katika hatua mbalimbali za uendelezaji na wawekezaji wanakaribishwa kushirikiana na STAMICO ili kufikia hatua ya uchimbaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mbali na miradi ya STAMICO, aliyataja baadhi ya madini muhimu ni lithium, graphite, iron, phosphate nickel, rare earth element (REE), cobalt, shaba.
“Lengo la jukwaa hili ni kukuza ushirikiano wa kikanda na kuvutia wawekezaji kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo ya madini,” alisema.
Moja ya mikakati ya Serikali kuendeleza madini muhimu nchini ni kupata taarifa za kina za kijiolojia kwa kufanya utafiti wa kina kupitia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) ili kuvutia uwekezaji nchini hasa katika hatua ya utafutaji madini mbalimbali.
“Hivi sasa utafiti wa aina hii nchini umefanyika kwa asilimia 16 tu, programu hii ni moja ya masuala muhimu yatakayotekelezwa kupitia “Vision 2030-Madini ni Maisha na Utajiri,” aliongeza Mhandisi Samaje.
Alifafanua kuwa, upatikanaji taarifa za kina za kijiolojia kupitia programu ya “Vision 2030 utasaidia kuyatambua maeneo yenye viashiria vya madini mbalimbali.
Lengo ni kuhakikisha tafiti za kina kama uchorongaji zinafanyika katika maeneo hayo ili kubainisha uwepo wa mashapo ya madini yanayoweza kuchimbwa kibiashara.
“Upatikanaji taarifa za kijiolojia katika maeneo ya wachimbaji wadogo utasaidia wachimbe kwa tija bila kupoteza mitaji yao.
“Pia taarifa zinazopatikana zitatumiwa na Wizara, taasisi nyingine za Serikali kama Wizara ya Maji kujua maeneo yenye miamba yenye mikondo ya maji chini ya ardhi kwa matumizi mbalimbali,” alieleza.
Jukwaa hilo limendaliwa na Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Ubalozi wa Uingereza Tanzania.
Sekta za umma na Serikali kutoka Tanzania Bara na Visiwani zinazoshiriki katika jukwaa hilo ni pamoja na Sekta Viwanda, Kilimo, Madini, Nishati, Uchumi wa Buluu, Fedha, Uwekezaji na Biashara.
Upande wa Sekta ya Madini, ujumbe wake unaongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara, Kheri Mahimbali, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia, Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba.
Wengine ni Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Augustine Olal, Kamishna Msaidizi wa Madini, Mhandisi Ally Samaje na Mchumi, Aman Ng’oma.