Na Mwandishi Wetu
WAKATI wowote linapotajwa jina la Samia Suluhu Hassan, kwa wenye fikra na akili timamu zinakuja kumbukumbu za utulivu na maridhiano kwenye nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambako Samia ndiye rais wa nchi.
Rais wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Mzee Ali Hassan Mwinyi alipata kutamka kuwa kila kitabu na zama zake.
Tanzania tangu ikiitwa Tanganyika imeshuhudia awamu sita sasa ikianzia na Mwalimu Julius Nyerere, Mzee Ali Hassan Mwinyi, Mzee Benjamin Mkapa, Mzee Jakaya Kikwete, Dkt. John Magufuli na sasa Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kila awamu ilikuwa na mazuri au mabaya ambayo wananchi waliyazungumza mitaani, lakini kubwa na la kipekee kwa Dkt. Samia ni kuweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo wa juu zaidi nchini Tanzania.
Pia anakuwa rais wa pili wa Tanzania kutokea Zanzibar, wa kwanza akiwa Mzee Ali Hassan Mwinyi aliyeliongoza taifa hilo kwa miaka 10 kutoka mwaka 1985 mpaka 1995.
Sifa moja kubwa ambayo watu waliowahi kufanya naye kazi wanaisema na ambayo si watu wengi wa nje wanaifahamu ni uwezo wake mkubwa wa kiuongozi. Yaani kusikiliza na kupokea ushauri kwa lengo la kuimarisha kitu chochote.
Si muongeaji sana bali ni msikilizaji wa muda mrefu. Pindi anapofanya maamuzi basi anakuwa amejiridhisha kwa pande zote, pia si muoga wa kukosolewa pale inapobidi kufanyika hivyo kwa maslahi ya pande zote.
Huyu ndiye Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ni sehemu ya marais saba wa nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC na Sudani ya Kusini.
Aidha, Rais Samia anaelezwa kama mwanasiasa anayependa kufanya maamuzi kupitia kusikiliza kila mmoja na si mtu wa kuamua mambo kwa pupa au kwa kuonea wengine; kwa sababu tu kuna mtu alimpelekea maneno ya chini chini.
Hili lilijionyesha zaidi wakati akiwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba katika mwaka 2014, ambapo wengi walivutiwa na mijadala aliyoibua na namna alivyokuwa akiwapa nafasi wajumbe kuzungumza kwa namna yoyote wawezavyo; hata wale ambao wengi walidhani serikali isingevutiwa na maoni yao kutokana na chembe chembe za upinzani, lengo lake likiwa mwisho wa kikao kipatikane kitu chenye sura ya kitaifa.
Huenda hapo ndipo nyota yake ilipong’aa. Ingawa Rais Samia kwa wanaomjua tangu zamani ni mtu aliyeifanyia makubwa nchi yake kwa Bara na Visiwani.
Itakumbukwa akiwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne, Rais Samia alishirikia kwa kiasi kikubwa vikao nyeti vya maamuzi juu ya mustakabali wa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Hata marekebisho ya mambo yaliyoitwa Kero za Muungano, kuna mkono na kauli zake kwenye mabadiliko hayo. Ingawa wengi hawajui.
Kwa kauli yake, Rais Samia alieleza namna alivyopambana katikati ya wanaume tena wazito akiwemo aliyekuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita Zanzibar, Amani Abeid Karume na Rais wa Awamu ya Nne Tanzania, Jakaya Kikwete.
“Nilikuwa mwanamke peke yangu lakini katika vikao nilisimama kwa nafasi yangu ya Waziri wa Muungano, wengi waliniuliza kama siogopi lakini nashukuru kaka yangu Rais Karume (Amani Abeid Karume) alinipa moyo akaniambia kama hiki unachokisema unakiamini basi kisimamie nami nitakuunga mkono,” alisema Rais Samia.
Ukweli wa historia yake ulijidhihirisha baada ya kushika madaraka ya urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo Machi 2021. Aliikuta nchi imegawanyika vipande vipande, vyama vya siasa vimepoteza matumaini na wafanyabishara wamekata tamaa.
Baadhi wamekimbia nchi wakiwemo wawekezaji na wanasiasa, kwa hofu ya kukamatwa au kuuwawa.
Akaja na kitu alichokipa jina la 4R (Reconciliation, Resilience, Reforms na Rebuilding). Ambapo kwa lugha ya Kiswahili R hizo nne zinasemwa ni Maridhiano, Ustahamilivu, Mageuzi na Ujenzi mpya wa Taifa.
Huenda watu wakachukulia hizi R nne kama kitu cha kitaifa pekee, lakini ukitazama kwa jicho pana zinaweza kutumika kote duniani wachilia mbali kwenye ukanda wa Afrika Mashariki hasa ikizingatiwa imekuwa ikipitia kipindi kigumu kwa nyakati tofauti kadiri viongozi wanavyobadilika kwenye nchi wanachama kwa sababu ya kumaliza muda wao au kufariki dunia.
Jumuiya ya Afrika Mashariki inazihitaji hizi R nne, kwa sababu nchi wanachama hawajakuwa na maridhiano ya pamoja katika baadhi ya mambo muhimu juu ya namna bora ya kuendesha jumuiya hii.
Kunahitajika ustahamilivu, kwa kuwa kila nchi mwanachama inajiona ina haki zaidi ya mwenzie. Kujiona bora na kuringia mipaka yake kumesababisha mambo mengi kuchelewa kutekelezeka.
Vilevile kunahitajika ustahamilivu baina ya nchi wanachama, kusameheana na kuona sote ni ndugu tuliotenganishwa na mipaka. Tunahitaji kustahamiliana kwenye maeneo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa ili tusonge mbele.
Pia nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zinahitaji mageuzi makubwa. Lazima kufanyike kitu kipya kuondoa kasumba na mambo yaliyozoeleka kila siku.
Kama nilivyoeleza hapo juu kuwa jumuiya hii imeanza mbali. Imeanza kuzeeka sasa na inahitaji mawazo mapya. Mawazo ambayo huenda yakawaumiza baadhi ya wanachama lakini baadaye yatakuwa na tija kubwa kwa wote.
Kitu cha mwisho katika hizi R nne kinachohitajika kwenye uimarishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ujenzi mpya.
Jumuiya inahitaji kujengwa upya, kuangalia fursa mpya zilizopo na namna bora ya kuziendea kwa lengo la kuleta mabadiliko.
Haya yote yanawezekana chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan aliyeamua kuja na kitu cha kipekee, kitu kinachoonyesha yupo tayari kubadilika na kushawishi wengine kubadilika ili waendane na wakati.
Huo ni ujasiri mkubwa ambao unakosekana kwenye nyoyo za viongozi wa Afrika ambao kwa asilimia kubwa wamekumbatia mambo ya zamani bila kutaka mabadiliko.
Kwa sababu dunia inakwenda kasi kwenye teknolojia mbalimbali kuanzia ya viwanda, kilimo na usafirishaji.