Samia alivyofanikiwa kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi

Na Daniel Mbega, Lindi

KUCHOCHEA Uchumi Shindani na Shirikishi ni moja ya vipaumbele vikuu vya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ambavyo vimo katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26.

Utekelezaji wa kipaumbele hiki ni mojawapo ya chachu zilizochechemua uchumi wa Tanzania ambao, kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia ya mwezi Septemba 2023 inayosema ‘Tanzania Economic Update 2023’, umeendelea kuhimili vyema athari za Uviko-19 na changamoto zingine za dunia zilizojitokeza katika miaka mitatu iliyopita.

Kulingana na taarifa hiyo ya Benki ya Dunia, pamoja na changamoto zilizojitokeza uchumi wa Tanzania umeendelea kuimarika kutokana na sababu kuu tatu, mojawapo ikiwa ni kuchochea na kuimarisha ushindani katika uchumi kwa muktadha wa kipaumbele cha Uchumi Shindani na Shirikishi.

Sababu ya pili ni kuendelea kuboresha na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuendelea kuaminiwa na taasisi za fedha duniani, pamoja na wadau wa maendeleo.

Mafanikio hayo yote ni jitihada za makusudi zinazofanywa na Serikali ya Samia, ambayo inaendelea kukua diplomasia ya uchumi na kujenga mazingira bora na wezeshi ya biashara na uwekezaji, ambayo yanaleta tija kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Kama alivyosema Profesa Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, wakati akiwaslisha Bungeni Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2024/25, katika kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa na athari chanya katika kuinuia kiwango cha miasha ya watu na kupunguza umaskini, mipango ya muda mrefu na mfupi ijayo itajikita kuhakikisha ukuaji wa uchumi unakuwa jumuishi, unapunguza umaskini, unazalisha ajira nyingi, unatengeneza utajiri na unachochea mauzo ya bidhaa zilizoongezwa thamani nje ya nchi.

“Ili kufikia azima hii, mkazo mahususi utawekwa katika sekta za uzalishaji ambazo zinahusisha watu wengi. Mkazo wa kipekee utawekwa katika kuchochea maendeleo kijamii na kiuchumi vijijini (rural socio-economic development),” anasema Prof. Kitila kwenye hotuba yake.

Kwa ujumla, Mapendekezo ya Mpango huo wa Maendeleo yamezingatia maudhui ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26, mpango ambao umetokana na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063; Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030 na mipango mingine ya kikanda.

Hali ya uchumi inaimarika

Taarifa za Beki Kuu ya Tanzania zinaeleza kwamba, mwaka 2022 thamani halisi ya Pato la Taifa (GDP) kwa Bei za Mwaka 2015 ilikuwa shilingi trilioni 141.9, ikilinganishwa na shilingi trilioni 135.5 mwaka 2021, likiwa ni ongezeko la asilimia 4.5.

Inaelezwa pia kwamba, kiwango halisi cha ukuaji kilikuwa asilimia 4.7 mwaka 2022 ikilinganishwa na asilimia 4.9 mwaka 2021, ikiwa ni pungufu kwa asilimia 0.2.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Prof. Kitila, kiwango cha ukuaji wa uchumi kinatarajiwa kuwa asilimia 5.2 mwaka 2023 na asilimia 6.1 mwaka 2024.

Ukuaji huo unatokana na jitihada za Rais Samia katika kuendelea kukabaliana vyema na athari zilizosababishwa na Uviko-19, pamoja na mikakati thabiti ya kukabiliana na athari za vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Aidha, inaelezwa pia kwamba ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa na uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu ya nishati, maji, afya, elimu, barabara, reli na viwanja vya ndege; kuongezeka kwa uzalishaji wa madini, hususani makaa ya mawe; kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi iliyochagiza shughuli za kiuchumi; na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi.

Kulingana na taarifa ya BoT ya mwezi Juni 20232, shughuli za uchumi zilizokuwa na mchango mkubwa katika Pato la Taifa ni pamoja na: kilimo (15.9%); ujenzi (15.5%); madini (11.9%); biashara na matengenezo (9.8%); na uzalishaji viwandani (9.0%).

“Mwaka 2022, mfumuko wa bei uliongezeka na kufikia asilimia 4.3 ikilinganishwa na asilimia 3.7 mwaka 2021. Katika kipindi kilichoishia Septemba 2023, mfumuko wa bei ulipungua na kufikia asilimia 3.3 ikilinganishwa na asilimia 4.7 katika kipindi kama hicho mwaka 2022.

“Kwa ujumla, mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia tatu (3%) hadi saba (7%). Hali hii imetokana na kuongezeka kwa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma na kuongezeka kwa upatikanaji wa mazao ya chakula nchini,” anasema Prof. Kitila.

Uchunguzi unaonyesha kwamba, uchumi wa Tanzania umekuwa ukikua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 6 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Aidha, uchumi wa Tanzania ulionyesha hali kubwa ya ustahimilivu hata katika kipindi cha misukosuko mikubwa ya kiuchumi duniani, ikiwemo wakati wa janga la ugonjwa wa Uviko-19 ambapo Tanzania haikufunga mipaka yake, na vita vinavyoendelea kati ya Urusi na Ukraine.

Kwa ujumla, shughuli za uchumi zimekuwa zikiongezeka katika maeneo na maisha halisi ya Watanzania.

Inaelezwa pia kwamba, katika kipindi cha miaka 20 iliyopita aina ya bidhaa zinazouzwa nje na nchi ambazo Tanzania inafanya nazo biashara zimebadilika sana.

Inaelezwa kuwa, miaka 20 iliyopita Tanzania iliuza zaidi mazao ya kilimo wakati sasa mauzo ya nje yanatawaliwa zaidi na mauzo ya madini.

“Miaka 20 iliyopita tuliuza zaidi bidhaa zetu katika masoko ya Ulaya, Marekani na Afrika, lakini kwa sasa tunauza zaidi katika masoko ya nchi za Asia (China, India, n.k.) na Mashariki ya Kati,” anasema Prof. Kitila.

Tathmini ya utekelezaji

Taarifa zinasema, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa 2022/2023 na wa mwaka 2023/2024 ulizingatia vipaumbele vitano kama ilivyokuwa katika miaka iliyotangulia.

Vipengele hivyo ni pamoja na: kuchochea uchumi shindani na shirikishi, kuimarisha uwezo wa uzalishaji na utoaji wa huduma, kukuza uwekezaji na biashara, kuchochea maendeleo ya watu, na kuendeleza raslimali watu.

Kwa maana nyingine, Serikali ya Rais Samia ilitekeleza miradi na programu mbalimbali katika kufikia malengo hayo.

Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa, katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji katika sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini hatua mbalimbali zimechukuliwa.

Hizo ni pamoja na kuongeza matumizi ya mbolea kwa asilimia 46, kutoka tani 363,599 mwaka 2021/2022 hadi tani 531,091 mwaka 2022/2023; kuongeza eneo la umwagiliaji kwa hekta 300,000 na hivyo kufikia hekta 800,000 za umwagiliaji kati ya hekta milioni 1.2 ambalo ni lengo lililowekwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano; kukamilisha ujenzi wa majosho 246 na ununuzi wa chanjo za mifugo milioni 696.4; na kuanza kwa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa Masoko.

Utekelezaji wa mipango hiyo umeleta tija kubwa kwa taifa ambapo kuna mafanikio mengi yamepatikana.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 17,148,290 mwaka 2021/2022 hadi kufikia tani 20,402,014 mwaka 2022/2023, likiwa ni ongezeko la asilimia 19 katika kipindi cha mwaka mmoja.

Hali hiyo ndiyo iliyokuwa inampa ujasiri Rais Samia wa kusema Tanzania inaweza kulisha Afrika katika miaka michache ijayo, kwani imeimarisha hali ya usalama wa chakula nchini ambapo hali ya utoshelevu wa chakula imefikia asilimia 124 mwaka 2022/2023 ikilinganishwa na lengo la kufikia asilimia 130 ifikapo mwaka 2025/2026.

Aidha, hali ya masoko ya mazao ya wakulima imeimarika ambapo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (National Food Reserve Agency-NFRA) na Bodi ya Mazao Mchanganyiko (CPB) wamenunua jumla ya tani 62,558.584 za mazao mbalimbali kutoka kwa wakulima.

Pia, kuongezeka kwa fedha za kigeni kutokana na mauzo ya madini kutoka Dola za Kimarekani bilioni 3.1 mwaka 2021 hadi Dola za Kimarekani bilioni 3.4 mwaka 2022, na kuchangia asilimia 56 ya mauzo yote ya nje, ikilinganishwa na lengo la kuchangia asilimia 50.5 lililowekwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

Katika kutimiza azima yake ya kuyaendeleza mema aliyoyakuta wakati anaingia madarakani, Rais Samia ameendelea na utekelezaji wa miradi ya kielelezo ya ujenzi wa miundo mbinu nchini, ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Ujenzi wa reli hiyo utakapokamilika utakuwa moja ya nyenzo kubwa katika Sekta ya Uchukuzi Tanzania itakayotoa mchango katika sekta hiyo kwa kuitumia fursa ya kijiografia iliyopo.

Mradi huo unaogharimu jumla ya shilingi trilioni 23.3 unahusisha awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni ujenzi wa reli kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza yenye vipande (lots) vitano: Kipande cha 1: Dar es Salaam – Morogoro (KM 300); Kipande cha 2: Morogoro – Makutupora (KM 422); Kipande cha 3: Makutupora – Tabora (KM 368); Kipande cha 4: Tabora – Isaka (KM 165); na Kipande cha 5: Isaka – Mwanza (KM 341).

Awamu ya pili inahusu ujenzi wa reli kutoka Tabora hadi Karema yenye urefu wa KM 1,010 ambayo itajengwa katika vipande (lots) vitatu: Kipande cha 1: Tabora – Kigoma (KM 411); Kipande cha 2: Uvinza – Musongati – Gitega (KM 282); na Kipande cha 3: Kaliua – Mpanda -Karema (KM 317).

Kumbukumbu zinaonyesha kwamba, hadi mwezi Aprili 2021, wakati serikali ya awamu ya sita inaingia madarakani, ujenzi wa reli hiyo ulikuwa katika vipande viwili vya Dar es Salaam – Morogoro (83.5%) na Morogoro – Makutupora (57.57%) na malipo yenye thamani ya shilingi trilioni 4.4 (kati ya shilingi trilioni 7.4) yalikuwa yamefanyika.

Lakini hadi kufikia Septemba 2023, ujenzi wa kipande cha kwanza umefikia asilimia 98.60 na kipande cha pili umefikia asilimia 95.41 na malipo yamefikia shilingi trilioni 6.3.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita imeanza ujenzi wa vipande vingine vipya vitano: Makutupora – Tabora ambao umefikia 12.32%; Isaka – Mwanza (37.20%); Tabora – Isaka (4.10%); Tabora – Kigoma (KM 506) na Uvinza – Gitega (KM 367) ambao upo katika hatua ya manunuzi.

Katika kuchochea uchumi shindani na shirikishi, pamoja na hatua zingine, Serikali ya Samia imekwisha kamilisha mchakato wa kupata mwekezaji wa kuwekeza, kuendeleza na kuendesha Bandari ya Dar es Salaam.

Itakumbukwa kwamba, baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi (IGA) kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mamlaka ya Falme ya Dubai mwezi Juni 2023, hatimaye Jumapili, Oktoba 22, 2023 mikataba mitatu ya utekelezaji wa miradi katika kuwekeza na kuendesha Gati za 0-3 na Gati za 4-7 ilisainiwa katika ya TPA na Kampuni ya DP World.

Kwa hali hiyo, Serikali inatarajia kuwa mapinduzi makubwa ya kiuwekezaji, kiuendelezaji na kiutendaji yatatokea katika Bandari ya Dar es Salaam katika siku chache zijazo.

Aidha, katika kukuza biashara na uwekezaji, pamoja na hatua zingine, Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.

Taarifa zinasema, kati ya Juni 2021 na Septemba 2023 jumla ya miradi 883 imesajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji ikiwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 12,154 (takriban Shs. trilioni 30.29) ambayo imezalisha ajira 160,107.

Inaelezwa kwamba, katika kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani, kiwango cha mauzo ya bidhaa za viwandani (manufacturing goods) kimeongezeka kwa asilimia 20.8, kutoka Dola za Kimarekani milioni 1,109.3 (Shs. bilioni 2.77) mwaka 2021 na kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,340.5 (Shs. bilioni 3.34) mwaka 2022 na baadaye kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,401.2 (Shs. bilioni 3.492) mwaka 2023.

Aidha, katika jitihada za Serikali ya Rais Samia kuchochea maendeleo ya watu, kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya msingi kilifikia asilimia 108.5 mwaka 2022, ikiwa ni zaidi ya lengo la kufikia asilimia 100 mwaka 2025/26.

Kumbukumbu zinaonyesha pia kwamba, kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa sekondari (Kidato cha I-IV) kimeongezeka kutoka asilimia 47.4 mwaka 2021 hadi asilimia 48.2 mwaka 2022, ikiwa ni zaidi ya lengo la kufikia asilimia 48 mwaka 2025/26.

Kiwango cha uandikishaji wa wanafunzi wa elimu ya sekondari (Kidato V – VI) kimeongezeka kutoka asilimia 6.7 mwaka 2021 hadi asilimia 7.6 mwaka 2022 ikiwa ni jitihada za kufikia lengo la asilimia 10 mwaka 2025.

Kwa upande wa afya, vifo vya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano vimepungua kwa asilimia 36 kutoka vifo 67 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 2015/2016 hadi kufikia vifo 43 kwa vizazi hai 1,000 mwaka 20224.

Jitihada za Samia zimesaidia pia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2014/15 hadi vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

Kwa upande wa sekta ya maji, utekelezaji wa miradi 630 yenye vituo 6,553 vya kuchotea maji vinavyonufaisha wananchi wapatao 4,393,274 kwenye vijiji 1,390 umekamilika.

Hii inafanya kiwango cha wananchi wanaopata maji safi na salama kufikia asilimia 88.6 mijini na asilimia 78 vijijini.

Aidha, katika sekta za huduma, mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na: Kuongezeka kwa idadi ya watalii kutoka watalii 1,711,625 mwaka 2021 kufikia watalii 3,818,080 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 123.1 ikiwa ni jitihada za kufikia lengo la watalii 5,000,000 mwaka 2025.

Pia kuongezeka kwa mapato ya utalii kutoka Dola za Kimarekani bilioni 1.31 mwaka 2021 kufikia Dola za Kimarekani bilioni 2.53 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 93.1 ikiwa ni jitihada za kufikia lengo la Dola bilioni 6.0 mwaka 2025.

Kwa ujumla, mafanikio hayo ni matokeo ya maamuzi sahihi ya Serikali ya Rais Samia, ya kupanga kwa muda mrefu, wa kati na mfupi, misingi thabiti ya uchumi na utekelezaji wa sera madhubuti za uchumi jumla, jitihada za makusudi za Serikali kujenga mazingira wezeshi na rafiki ili kuchochea shughuli za kiuchumi na maendeleo nchini pamoja na ushirikiano na wadau mbalimbali wa maendeleo katika utekelezaji wa ajenda ya maendeleo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *