Na Daniel Mbega
UNAFAHAMU kwamba mama anayetumia jiko la mkaa anapata madhara makubwa kuliko mtu anayevuta sigara? Au unafahamu kuwa kitendo cha kuwemo jikoni kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara 300 kama unapikia nishati ya kuni au mkaa?
Tafiti zinaonyesha kwamba, takriban watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati chafu ya kupikia, ikiwemo kuni, mkaa, mabaki ya mazao na kinyesi cha wanyama.
Wataalamu wa magonjwa ya njia ya upumuaji wanasema kwamba, nishati hizo zinazalisha kemikali ya monoksidi ya kaboni inayoathiri oksijeni kwenye seli mwilini. Kwa kifupi, mkaa na kuni ni magaidi wa siri walioko jikoni, ambao wanasababisha madhara makubwa hasa kwa wanawake, na hata vifo.
Kulingana na wataalamu, watu milioni 38.8 wanaishi wakiwa na magonjwa yanayotokana na matumizi ya nishati chafu, yaliyopo katika mfumo tofauti.
Madhara ya muda mrefu ya matumizi ya nishati hizo ni watu kupata ugonjwa wa ‘Pulmonary COPD’ unaosababisha kikohozi, mafua na maumivu kwenye mapafu, ambapo mishipa ya njia ya hewa ndogondogo inatanuka mtu anashindwa kupata hewa vizuri, imehusianishwa sana na wanaotumia kuni na mkaa COPD ni magonjwa ya mapafu yanayosababisha mirija ya hewa kushindwa kutanuka na kushindwa kubeba hewa vizuri.
Inaelezwa kwamba, kuni sumu yake inakuwa juu zaidi kwa kuwa moshi unaotoka unakuwa zaidi na Carbon dioxide inayosababisha damu kushindwa kusafirishwa kwenye oksijeni na hivyo kukata pumzi.
Kiwango cha kemikali kinatokana na moto uliowashwa, na anayetumia kuni au mkaa katika sehemu iliyofungwa ikiwemo kwenye banda au ndani ya nyumba athari yake ni kubwa zaidi.
Lakini hatari si kwa upumuaji pekee, bali hata macho ni shida, ambapo machozi yanayotokana na moshi husababisha macho kuywa mekundu. Ndiyo maana wale ndugu zetu wa Kanda ya Ziwa huwaua wazee wenye macho mekundu kwa madai kwamba ni wachawi kumbe ni athari ya matumizi ya nishati hizo.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema katika utafiti wake kwamba, moshi unaotokana na kuni za kupikia ni mojawapo ya visababishi vikuu vya vifo vya watoto wachanga duniani, vikigharimu maisha ya watoto 500,000 chini ya miaka mitano kila mwaka.
Utafiti huo unachambua matumizi ya nishati hizo na kuenea kwa magonjwa ya kupumua kwa watoto hao kupitia tafiti 41 zilizofanywa katika nchi 30 zinazoendelea kutoka bara la Asia, Afrika na Amerika ya Kusini.
Matokeo yalipendekeza jamii kuweka nje majiko yanayotumia nishati hizo ambapo tafiti zinaonyesha takriban watu bilioni tatu katika nchi zinazoendelea wanategemea kuni au mkaa kwa ajili ya kupikia.
Kwa mujibu wa WHO magonjwa yanayosababishwa na moshi husababisha vifo vya watu milioni 4.3 kila mwaka vikiupiku ugonjwa wa Malaria na Kifua Kikuu.
Marufuku ya Serikali
Hali hiyo ndiyo iliyoifanya Serikali ya Awamu ya Sita kuja na mkakati wa kupiga marufuku matumizi ya kuni na mkaa, kwa kuanzia kwenye taasisi.
Mnamo Aprili 12, 2023, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jafo, alisema kwamba, taasisi zote ambazo zinahudumia watu wasiopungua 100, mwisho wao wa kutumia kuni na mkaa utakuwa ni Januari 31, 2024 na wanaohudumia watu kuanzia 200 mwisho wao ni Januari 31,2025.
Waziri Jafo amesema zaidi ya Hekta 46,960 ambayo ni asilimia 26 ya ardhi huharibiwa kila mwaka kutokana na ukataji wa miti kwa matumizi ya kuni na mkaa jambo ambalo ni hatari kwa kuwa linamaliza misitu.
Inaelezwa kwamba, inakadiriwa kuwa asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizoendelevu ikiwemo kutumia nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia.
Nishati ya kuni hutumika kwa wingi kwa sababu ni rahisi kupatikana na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake tofauti na nishati nyinginezo kama vile umeme na gesi.
Hata hivyo, licha ya unafuu wake lakini upatikanaji wa nishati hiyo na matumizi yake yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu inayoathiri mapafu, moyo na magonjwa ya kupumua kwa watoto.
Kwahiyo Serikali imeweka mkakati wa kupunguza athari hizo kwa kuandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.
Katika nchi nyingi za Kusini mwa Janga la Sahara, njia kuu ya kupika ni kwa kutumia mkaa, kuni na mafuta ya taa.
Kwa mujibu wa shirika la Clean Cooking Alliance, watu milioni 950 wanategemea kuni na mkaa kupikia, idadi inayokadiriwa kukua hadi bilioni 1.67 ifikapo 2050.
Njia hizi za kupikia hutumiwa sana kutokana na kuwa nafuu kwa familia nyingi za kipato cha chini.
Katika meneo ya mjini na vijijini, ni kawaida kukuta majiko ya kupikia yenye mkaa kwenye makazi yao.
Lakini njia hizi za kupikia huwa na madhara ya muda mrefu ya kiafya kwa mujibu wa wataalamu.
Kuna athari za kiafya kwa wazalishaji wa mkaa na watumiaji. Mkaa kimsingi ni kaboni tupu, na mkaa unaochomwa hutoa viwango vya juu vya kaboni dioksidi, kaboni monoksidi, na vichafuzi kama vile masizi, ambavyo vinaweza kuingia ndani kabisa ya mapafu, hasa katika majiko yasiyokua na sehemu za kutolea hewa ya kutosha.
Uzalishaji huu unaweza kuwa na madhara sana, kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO karibu watu milioni 4 kote ulimwenguni hufa kabla ya wakati kila mwaka kutokana na kupikia kwa moto na nishati ngumu kama mkaa.
Watafiti wanaongeza kuwa huenda athari ikawa kubwa zaidi kutokana na kutokua na takwimu za kutosha katika nchi hizi za kusini mwa janga la Sahara.
Kumbukumbu ya vifo
Katika miaka ya 1990 kulikuwa na mfululizo wa vifo vingi hasa Nyanda za Juu Kusini (mikoa ya Iringa na Mbeya) – wakati huo mikoa ya Njombe na Songwe ilikuwa haijaanzishwa bado.
Mara nyingi vifo hivyo vilitokea nyakati za usiku na haikuwa ajabu kusikia kwamba familia nzima imepoteza maisha ‘katika hali ya kutatanisha’.
Awali vifo hivyo vilileta ukinzani hata katika vyombo vya usalama wakati wa upelelezi na wale wenye Imani haba hawakusita kuvihusisha vifo hivyo na ushirikina.
Hata hivyo, uchunguzi wa kitaalamu baadaye ulibainisha kwamba vifo vingi vilisababishwa na majiko ya mkaa ambayo waliyawasha na kujifungia nayo ndani ili yalete joto kutokana na hali ya hewa ya baridi kali katika mikoa hiyo, hasa nyakati za kipupwe.
Wengi hawakuelewa. Iweje majiko yasababishe maafa wakati ambapo yaliwashwa tu, yakawekwa chumbani na hakuna hata cheche zilizosababisha moto?
Jibu ni rahisi sana. Mkaa tunaopikia unatoa hewa-ukaa (carbon dioxide – CO2) na wakati unapokuwa umewashwa unanyonya hewa ya Oksijeni ambayo viumbe hai, hususan binadamu na hayani wengine, wanaivuta na kutoa nje hewa-ukaa (CO2).
Kwa maana nyingine, mkaa unapowashwa unakuwa unanyang’anyana hewa ya Oksijeni na binadamu, na pindi milango na madirisha yanapokuwa yamefungwa – kama ilivyokuwa inatokea wakati huo kwenye Nyanda za Juu Kusini, hewa ya Oksijeni inakuwa ndogo na hewa-ukaa ndiyo inazidi, hivyo kumfanya mtu kuishiwa pumzi, kuishiwa nguvu na hatimaye kupoteza maisha ikiwa hatapata msaada wa haraka.
Wengi tunajua kwamba vyakula vingi vya viwandani vilivyowekwa kwenye makopo na makasha ya paketi si salama kwa asilimia 100, na pia wengi hujua kwamba vinywaji laini na pombe sio salama kwa asilimia 100, pia wengi tunajua sindano na vidonge vya uzazi wa mpango si salama kwa asilimia 100. Pia vyakula vingi fresh vya kutoka nje ya nchi kama samaki, na nyama na jibini siyo salama kwa asilimia 100.
Lakini wengi hatujui kama MAJIKO yetu tunayotumia (hususan ya mkaa) si salama kwa asilimia 100 kama ilivyoelezwa hapo juu.
Mara nyingi ukiletewa chakula mezani, fikiria kidogo na jiulize swali hili: “Chakula nilacho kinaenda kuufanyaje mwili wangu?” Au jiulize, “mpishi alitumia nishati gani na alikaa kwa muda gani?”
Ni dhahiri kwamba, wanawake – ambao ndio daima hukaa jikoni kupika – wako hatarini kiafya kwa sababu ya ‘gaidi’ anayeitwa ‘Jiko la Mkaa’ ambaye anawafyonza kinga na kuwasababishia madhara mengi kiafya.
Angalizo dogo
Wagonjwa wengi wa magonjwa sugu wamekuwa wakilalamika mara kwa mara kwamba ametumia dawa fulani ya kampuni fulani akapata nafuu lakini hakuweza kupona kabisa.
Akinamama kwa akinababa wengine pia walitumia mbinu mbalimbali za kupunguza uzito na kufanikiwa lakini baada ya muda uzito ulirudi tena mara mbili zaidi.
Swali ni kwamba nini shida. Jibu ni rahisi sana. Ukishatibiwa malaria unatakiwa ulale kwenye chandarua chenye dawa, siyo ulale bila chandarua. Ukilala nje ya chandarua utapata malaria tena.
Ndiyo, hata ugonjwa sugu ukishatibika au kupata nafuu basi unatakiwa uache baadhi ya vitu vilivyosababisha wewe kupata magonjwa hayo.
Kuna madhara makubwa kwa wanawake yanayoababishwa na utumiaji wa majiko ya mkaa, miongoni mwake ni kuathirika ama kuvurugika kwa homoni za kike.
Dalili kwamba homoni za mwanamke zimevurugika
1. Kuwa na hedhi ya muda mrefu zaidi ya siku 7
2. Kuwa na hedhi yenye kuambatana na maumivu Makali sana
3. Kuwa na hedhi yenye kuambatana na kichefu chefu na kuharisha
4. Kuwa na hedhi iliyojaa woga mkubwa sana
5. Kuwa na hedhi ambayo haina mpangilio, Unaweza kuingia mara tatu kwa mwezi mmoja, mara mbili au unaweza usipate kabisa hata miezi 6 hadi mwaka.
6. Kuwa na ndevu sehemu za usoni na kifuani nyingi kupita kiasi
7. Kuwa na kitambi cha tumbo la chini (Abdominal obesity)
8. Kukosa mtoto kwa muda mrefu
9. Kukosa hamu ya tendo la ndoa na kuwa na tendo la ndoa lenye kuambatana na maumivu makali
10. Mwili kuwa unauma sana hasa misuli bila sababu ya msingi, kuumwa sana na kichwa bila sababu ya msingi.
Homoni ni vitu gani
Homoni ni kemikali zinazotolewa na tezi za mwili na kusafiri mwilini kupitia mfumo wa mzunguko wa damu hadi ogani za mwili. Homoni ndio zinasababisha mabadiliko katika ogani mbalimbali za mwili. Kwa lugha nyingine zinapeleka ujumbe kwa ogani mbalimbali za mwili ili ziweze kufanya kazi kulingana na mahitaji ya mwili.
Homoni ndio kemikali kuu zinazotumika kusafirisha taarifa kwenye viungo mbalimbali vya mwili hivyo mabadiliko madogo ya homoni husababisha mabadiliko makubwa kwenye mwili.
Mfumo wa utengenezaji wa homoni unalingana kwa kiasi kikubwa kwa wanaume na wanawake isipokuwa homoni zinazotengenezwa kwenye tezi zilizopo kwenye mfumo wa uzazi.
Baadhi ya Homoni na kazi zake
1. Homoni ya Kiume – Testosteroni, homoni hii huhusika na uumbaji wa via vya uzazi tangu mtoto akiwa tumboni, inabalehesha na pia kumpa mwanaume nguvu na hamu za tendo la ndoa. Katika mwili wa mwanamke homoni hii ipo kidogo sana.
2. Homoni ya Kike – Oestrogen, homoni hii huhusika na uumbaji wa via vya uzazi vya mwanamke tangu akiwa tumboni, inabalehesha na pia inahusika na mzunguko wa hedhi na kumpa mwanamke hamu ya tendo la ndoa.
3. Homoni ya Insulini – homoni hii ipo kwa wanaume na wanawake inahusika na kupunguza kiasi cha wanga na sukari (glucose) katika mfumo wa damu.
Namna homoni zinavyovurugwa
Miili yetu ikiwa katika hali ya kawaida hutengeneza homoni kwa uwiano stahiki na kufanya ogani na tishu za mwili kufanya kazi vizuri.
Pale homoni moja au zaidi inapoongezeka au kupungua kiwango cha kawaida kinachohitajika na ogani/tishu ili kuweza kufanya kazi basi na homoni zingine huongeza au kupunguza uzalishaji wake.
Baadhi ya sababu zinazopelekea kuvurugika kwa hormone mwilini.
– mifumo ya uzazi wa mpango wa kisasa (vidonge na vijiti)
– msongo wa mawazo
– matumizi makubwa yaliyopitiliza ya vipodozi.
– ujauzito, kukoma kwa hedhi kwa wanawake kutokana na umri
– kubale/kuvunja ungo
– kutokufanya mazoezi
– mfumo wa maisha, unene, na mfumo wa ulaji (kula wanga na sukari ile hali wanga huo hauendi kutumika).