Na Daniel Mbega
Kisarawe
ULINGO wa Kwae haulindi Manda! Naam. Haya ni maneno kuntu ya mamanju wa Kiswahili, wakimaanisha kwamba, mtu anayeamia ndege au koko (kima) kwenye shamba lililoko Kwae, hawezi kuamia katika shamba lililoko Manda kwa wakati mmoja.
Kwa wasiojua tu ni kwamba, Kwae na Manda ni vijiji vya zamani katika Kisiwa cha Lamu nchini Kenya. Kwae iko jirani na eneo la Burujini na Kijiji cha Kikomani, kaskazini mwa Manda. Manda ni kisiwa kidogo kilichokuwa maarufu kwa bandari za Takwa na Manda wakati wa karne ya 9.
Maeneo hayo mawili ni maarufu kwa kilimo cha mahindi, mihogo, ufuta na pamba, ingawa awali katika karne ya 19 yaliwahi kukimbiwa kutokana na uhaba wa maji kabla ya Serikali kujenga miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua na kuwafanya watu warejee tena kuweka makazi, hususan Manda ambako kuna uwanja wa ndege.
Msemo huu wa wahenga una mantiki kubwa, kwa sababu, kwa umbali uliopo baina ya maeneo hayo mawili, katu usitegemee mlinzi wa eneo moja akalinda na eneo jingine, tena likiwa mbali na kutenganishwa na maji.
Ndugu zangu Wamatumbi na Wandengeereko ambao ni mafundi wa kujenga maghorofa ya kienyeji (madungu) kwa ajili ya kuamia ndege kwenye mshamba ya mpunga ni mashahidi pia, kwamba hata ukisimama kwenye dungu lako huwezi kuamia kwa jirani.
Usemi huu wa wahenga ninaufananisha na uwekezaji unaotakiwa kufanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi na kukuza mapato.
Tayari mikataba mitatu ya uwekezaji na ukodishaji wa maeneo kadhaa ya Bandari ya Dar es Salaam imekwishasainiwa tangu Jumapili, Oktoba 22, 2023, ambayo sasa yataipa nafasi kampuni ya Dubai Port World (DP World) kuleta ufanisi kwenye bandari hiyo muhimu.
Wapo watu wanaohoji kwamba, iweje mwekezaji mkubwa kama DP World aanze na mtaji wa Dola milioni 250 pekee? Wengine wanasema, kiasi hicho cha fedha kingeweza kutolewa na wafanyabiashara wa ndani kama Rostam Aziz au Said Salim Bakhressa – ikibidi hata kwa kuchanga!
Lakini hawaelewi kwamba, kwanza kiasi hicho ni mtaji anzia, na kinaweza kuongezeka kadiri utekelezaji unavyoendelea. Pili, DP World hawaendi kujenga miundombinu, wanakwenda kuitumia iliyopo na kuongeza vitendea kazi vya kisasa, kwani gati hizo kuanzia Gati namba 4 – 7 zilikwishajengwa na Serikali yetu.
Jambo la muhimu ni kwamba, wanaotoa mawazo hayo wanashindwa kutambua kwamba, ukiacha kuwa na fedha, ni lazima uwe na utaalamu. Wafanyabiashara wa ndani wanaweza kuwa na fedha, sawa. Lakini hawana utaalamu na uzoefu wa shughuli hizi tofauti na ilivyo kwa DP World ambayo imewekeza katika nchi 68 duniani na inamiliki takriban meli 400 huku pia ikiwa na Bandari Kavu jijini Kigali, Rwanda, nchi ambayo inaihitaji Bandari ya Dar es Salaam kusafirishia mizigo yake.
Kuna wengine wanasema, badala ya kutafuta mwekezaji tunaweza kuiendesha wenyewe tu!
Hawa sasa ndio wanaoangukia kwenye msemo wa ‘Ulingo wa Kwae haulindi Manda!’ Unawezaje kuamia mashamba mawili yaliyoko mbalimbali kwa wakati mmoja?
Maana yangu ni kwamba, Serikali ina majukumu mengine mengi ya kuwaletea Watanzania maendeleo, inahitaji fedha – ambazo kama Bandari ikiwa na ufanisi wa kutosha zitapatikana.
Serikali hii, kwa kutumia mapato yake ya ndani na misaada ya wahisani na mikopo yenye masharti nafuu, inapambana usiku na mchana kuhakikisha huduma za kijamii zinapatikana – elimu, maji, afya, umeme, miundombinu na kadhalika.
Sasa watu wanaposema Serikali yenyewe ndiyo isimamie Bandari, halafu mtegemee ufanisi, ni sasa na kumtaka Mkumba aambie shamba na Mbonde kutokea kwenye dungu lake!
Kwanza, kama Rais Samia Suluhu Hassan alivyosema wakati wa hafla ya utiaji saini mikataba hiyo Ikulu jijini Dodoma, Watanzania wote wanafahamu fika pale bandarini kuna changamoto ambazo hutofautiana namna ya kuzitatua, ingawa wapo wanaoamini bila mbia zinaweza kutatuliwa licha ya kuwa mbali kiuhalisia.
Binafsi naungana na Rais Samia kuwa, njia ambayo baadhi walitaka tuitumie, ya kutohitaji wabia, itachukua muda mrefu sana kufika wakati dunia inakwenda mbio sisi tungekuwa bado tunasuasua.
Lakini pia, tulishajaribu lakini hatukufanikiwa, ndiyo maana hata kabla ya ujio wa DP World alikuwepo mwekezaji mwingine, kampuni ya Hutchison Ports ya Hong Kong ambayo ilianzisha kampuni tanzu nchini Tanzania ya Tanzania International Container Terminal Services (TICS). Mkataba wa kampuni hii umefikia kikomo mwaka 2022, tena baada ya kuiongezea miaka miwili badala ya 20 ya awali.
Kinachofurahisha katika uwekezaji huu wa DP World ni kwamba, ukomo wa mkataba ni miaka 30, tofauti na watu walivyokuwa wanavumisha awali, tena basi utakuwa ukirejelewa kila baada ya miaka mitano.
Serikali itakuwa na hisa kwenye kampuni itakayoanzishwa, tena basi imewekeza kwenye maeneo machache tu ya Bandari ya Dar es Salaam, siyo yote, na wala haihusishi bandari nyingine.
Mbali ya kwamba Sheria za Tanzania ndizo zitatumika na kwamba mkataba unaweza kusitishwa wakati wowote, lakini pia hakuna mfanyakazi hata mmoja wa Bandari atakayepoteza ajira, isipokuwa tu wanaweza kuamua ama kubaki Bandari au kujiunga na DP World wakitaka.
Haya yote yalipotoshwa. Na waliofanya mchezo huo wanafahamu kwanini walifanya hivyo wakati wanajua ukweli halisi ulivyo.
Kimsingi, mkataba huu umezingatia maoni ya wananchi kama alivyosema Rais Saia mwenyewe.
“Mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa kwa kupitia mmoja mmoja na makundi mbalimbali ya kijamii pamoja na sheria na taratibu zote za nchi.
“Niwape uhakika watanzania maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa, hakuna atakayepoteza kazi bandarini kutakua na kufuata mfumo ili viwango vikae sawa viendane na dunia, kukzua ufanisi na baishara na mapato ya nchi yetu,” alisema Rais Samia.
Kimsingi, Bandari ya Dar es Salaam ndiyo kiunganishi muhimu cha biashara na kuhudumia shehena kubwa ya mizigo kutoka nchi jirani na mataifa ya mbali, kwahiyo maboresho yatakayofanywa kupitia uwekezaji huo yatakuza biashara za ndani na nje na kuwezesha shughuli za kiuchumi za nchi jirani itakayoongeza maapto ya serikali na kukuiza uchumi wa taifa kwa ujumla.
Hii itaongeza mapato ya Serikali kutoka Shs. trilioni 7.8 zinazokusanywa eneo la bandari pekee mwaka 2021-2022 hadi Shs. trilioni 26.7 mwaka 2032, yaani miaka tisa kuanzia sasa.
Ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam utafanya bandari yetu ishindane kibiashara na bandari za Mombasa-Kenya, Beira-Msumbiji na Durban nchini Afrika Kusini.
Kwa ifupi, ninamhongera Rais Samia na timu yake kwa uamuzi sahihi alioufanya katika kuiboresha Bandari ya Dar es Salaam, ambayo ni ‘mgodi’ mama wa mapato ya Serikali.
Mgodi huu ukichimbwa vizuri, na usimamizi wa mapato ukawa mzuri, kuna matumaini makubwa mapato yatakuwa mengi na Serikali inaweza kuitegemea Bandari kwa asilimia 40 katika Bajeti yake Kuu.
Kijijini Msanga-Ngongele,
Kisarawe.
0629-299688