Na Daniel Mbega,
Dar es Salaam
JUNI 13, 2023 Benki ya Dunia iliiweka Bandari ya Dar es Salaam katika nafasi ya juu kuliko Bandari ya Mombasa kwenye orodha mpya ya bandari zenye ufanisi zaidi baada ya kipindi cha mpito cha janga la Uviko-19 na Vita vya Ukraine.
Hali hiyo ikaleta hofu ya ushindani ambayo Kenya imekuwa nayo juu ya Tanzania kuwa Mombasa ndiyo ilidaiwa kupendelewa kutumiwa na wasafirishaji.
Mbali ya Dar es Salaam, bandari za Djibouti na Berbera ya Somalia nazo ziliipita Mombasa kwa ufanisi.
Haya yamejiri wakati Bandari ya Dar es Salaam katika miaka ya karibuni imekuwa na ushindani mkubwa, na kutishia kuvuta meli nyingi zinazoingia katika bahari ya Afrika Mashariki.
Katika orodha hiyo, bandari ya Dar es Salaam ilirekodi kuimarika na kupanda kwa nafasi 49 kutoka nafasi ya 361 ya awali hadi kushika nafasi ya 312 mwaka 2021.
Toleo hilo la Tatu la Matokeo ya Utendaji kazi wa Bandari za Kontena duniani (Container Port Performance Index 2022) likaiweka Mombasa katika nafasi ya 326 kati ya bandari 348 duniani kote ambazo zilitathminiwa.
Kulingana na Ripoti ya Benki ya Dunia (Container Port Performance Index 2022), Bandari ya Mombasa iliporomoka mno tofauti na ilivyokuwa mwaka 2021 ambapo iliwekwa katika nafasi ya 296 na Benki ya Dunia.
Kuporomoka kwa ufanisi katika Bandari ya Mombasa ndiko kulikoifanya Serikali ya Rais William Ruto wa Kenya kuamua kutafuta mwekezaji binafsi kwenye sekta ya bandari, ambapo imepanga hadi kufikia Desemba 2023 iwe imempata na kumkabidhi bandari zake tano azisimamie na kuziendeleza.
Uwekezaji huo, kulingana na andiko maalum la mradi, utahusisha miradi mikubwa mitatu ya ujenzi katika Bandari za Mombasa na Lamu pamoja na Ukanda Maalum wa Kibiashara wa Lamu (Lamu SEZ).
Uamuzi wa Serikali ya Ruto umejikita katika mkakati wa kuongeza ufanisi kwenye bandari zake na kuliteka soko la nchi za Kaskazini zisizo na bandari, hasa Sudan Kusini na Ethiopia.
Taarifa za ndani zinaeleza kwamba, uamuzi wa Kenya umekuja kutokana na kuwepo kwa ushindani wa kibishara, hasa usafirishaji wa mizigo kutoka nje kwa nje zisizo na bandari kama Uganda, Rwanda na Burundi, ambazo zinaonelea ni vyema sasa kutumia njia ya Tanzania.
Fursa muhimu
Katika kipindi hiki cha ushindani wa kibiashara na haja ya kupanua wigo wa mapato, Serikali ya Tanzania imepiga hatua kumi mbele ya Kenya, hasa kwa kuazimia kupata mwekezaji wa kusimamia Bandari ya Dar es Salaam ili kuongeza ufanisi.
Kwa kifupi, Tanzania na Kenya zote zimeazimia kuboresha bandari zao, au kujenga bandari mpya (Ujenzi wa Bandari ya Lamu kwa upande wa Kenya na uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam kwa Tanzania), zikiwa zinapigania soko la wafanyabiashara wa nchi zisizo na bandari zinazosafarisha mizigo yao kutoka ama kupeleka nje.
Tayari Tanzania imekwishachagua kampuni ya DP World ya Dubai ili kuboresha bandari zake na kuleta ufanisi, lakini nayo Kenya imeamua kutafuta mwekezaji mahiri asimamie sekta hiyo ili kukuza uchumi wake.
Kulingana na andiko hilo la Hazina Kenya lililo katika ngazi ya majadiliano (Project Information Memorandum – PIM), mambo ambayo yanaangaziwa kuwekezwa ni Kituo cha Makasha katika Bandari ya Lamu Gati Namba 1-3 (Lamu Container Terminal Berth 1-3), Kanda Maalum ya Kibiashara ya Lamu (Lamu SEZ), na Ujenzi wa Gati nne katika Bandari ya Mombasa (Gati ya 11-14).
Mpango wa Ushoroba wa Lamu Port-South Sudan-Ethiopia Transport (LAPSSET) unatajwa kuwa ni kipaumbele kikubwa chini ya mkakati wa Dira ya Kenya ya mwaka 2030 ambao unalenga kuchochea ukuaji wa uchumi katika masoko ambayo hayajaendelea kwenye ukanda huo.
Mkakati wa Dira ya Kenya ya 2030 ni sera ya kitaifa ya maendeleo ya muda mrefu inayolenga kubadilisha Kenya kuwa nchi mpya ya viwanda, yenye kipato cha kati, kutoa maisha ya hali ya juu kwa raia wake wote ifikapo mwaka 2030 katika mazingira safi na salama.
Siyo siri kwamba, tangu Serikali ya Tanzania ilipoanza kuongeza juhudi za kuiboresha miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam kupitia programu ya Dar es Salaam Maritime Gateway Programme (DMGP), ufanisi wa bandari hiyo umeimarika sana.
Lakini mafanikio hayo ya Bandari ya Dar es Salaam, japokuwa yanatia moyo, bado hayajaleta ufanisi mkubwa ambao Serikali ya Awamu ya Sita inautaka.
Umuhimu wa kuharakisha
Kuyafikia malengo hayo ndiyo maana Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha marekebisho yanafanyika katika vipengele mbalimbali vya makubaliano na kampuni ya DP World ya Dubai.
Siyo siri, katika suala la kukuza mapato kupitia Bandari, ufanisi ni muhimu ukazingatiwa, na katika kipindi hiki ambacho Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine, iko kwenye ushindani kiuchumi, kuna umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji katika sekta hii, hususan Bandari ya Dar es Salaam, unaharakishwa ili malengo husika yaweze kufikiwa.
Kilicho bayana hapa ni kwamba, kwa kipindi cha miezi kadhaa sasa Serikali, kama alivyoahidi Rais Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikizirekebisha kasoro mbalimbali zilizoainishwa na wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla, ili kuhakikisha kwamba, utekelezaji wa mkataba baina ya DP World na Serikali unafanikiwa.
Serikali ya Awamu ya Sita, ambayo kimsingi inazingatia maslahi mapana ya Taifa, iko tayari kuyazingatia maslahi hayo kwenye mkataba huo, ambao kusainiwa kwake kutaleta tija kubwa katika uchumi.
Baadhi walikuwa na hofu kuhusu kuzingatiwa kwa maslahi hayo ya taifa, wamekuwa na hofu na ajira, wamekuwa na hofu kwamba mwekezaji atachukua ardhi, lakini ukweli ni kwamba hakuna atakayepoteza ajira, san asana ajira zaidi zitazalishwa. Pia hakuna mwekezaji anayeweza kupewa ardhi kwa sababu hata kwenye sheria za uwekezaji, mwekezaji hapewi ardhi bali anapata kibali cha kukaa juu ya ardhi, na analipa kodi.
Imekwishaelezwa mara kadhaa, na ushahidi upo wazi, kwamba DP World imewekeza kwenye nchi nyingi duniani na imejenga bandari kavu nchini Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Kampuni hiyo inahudumia bandari zaidi ya 168 duniani, ina meli zaidi ya 400. Meli hizi zitaleta mizigo kwenye bandari yetu na kwa ujumla uchumi wa Tanzania utafunguka.
Nchi zisizo na bandari kama Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi na Zambia zinaitegemea bandari hiyo na ufanisi utakapoongezeka hata mapato nayo yataongezeka.
Manufaa ya uwekezaji
Wakati mwingine kurudia kutaja faida za uwekezaji siyo vibaya, bali hiyo huleta msisitizo wa umuhimu wa kuharakisha uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam.
Wataalamu wamekwishasema mara kadhaa kwamba, zipo faida nyingi za DP World kuwekeza kwenye Bandari ya Dar es Salaam, lakini 12 kati ya hizo ni pamoja na kupunguza muda wa meli kukaa nangani kutoka siku 5 kwa sasa mpaka saa 24 tu.
Ikumbukwe kuwa, kadiri meli zilivyokuwa zikichelewa kupakua ama kupakia mizigo ndivyo ambavyo gharama zilikuwa zinaongezeka kutoka kwa wamiliki wa vyombo wenyewe, wafanyabiashara na hatimaye mzigo mkubwa wa gharama ulikuwa unamwendea mwananchi wa kawaida, mlaji, ambaye amekuwa akilazimika kununua bidhaa kwa bei ya juu kwa sababu wafanyabiashara wanafidia gharama zao, zikiwemo za kuchelewa kutoa mizigo.
Ujio wa DP World utaongeza idadi ya meli zitakazokuja Bandari ya Dar es Salaam kutoka meli 1,569 zilizohudumiwa mwaka 2021/22 hadi kufikia takriban meli 2,950 ifikapo mwaka 2032/33.
Hii maana yake ni kwamba, mizigo mingi itasafirishwa kwa wakati iwe inayotoka nje au inayoingia, tofauti na sasa. Na kwa kufanya hivyo mapato yataongezeka.
Ufanisi utakaoletwa na uwekezaji huo ni kupunguza muda wa ushushaji wa makontena kutoka wastani wa siku 4.5 mpaka siku 2. Kwa sasa wafanyabiashara wengi wanalia kutokana na muda mrefu wanaotumia, ambao unawaongezea gharama.
Lakini hii pia itapunguza gharama ya usafirishaji wa shehena kutoka nchi za nje kwenda nchi za jirani, kutoka USD 12,000 mpaka kati ya USD 6,000 na USD 7,000 kwa kasha.
Jambo kubwa na la msingi ni kwamba, shehena inayohudumiwa itaongezeka kutoka tani milioni 18.41 kwa mwaka 2021/22 hadi kufikia tani milioni 47.57 mwaka 2032/33. Hii pia itaongeza mapato ya serikali yatokanayo na kodi ya forodha inayokusanywa katika shehena inayopitishwa bandarini kutoka Shilingi trilioni 7.76 kwa mwaka 2021/22 hadi Shilingi trilioni 26.70 kwa mwaka 2032/33.
Fauka ya hayo, uwekezaji huo utaongeza ajira zinazotokana na shughuli za bandari kutoka 28,990 kwa mwaka 2021/22 hadi 71,907 ifikapo mwaka 2032/33.
Faida nyingine ni kupunguza muda wa uondoshaji mizigo kutoka saa 12 mpaka saa 1 tu kutokana na uboreshaji wa mifumo yạ Tehama, pia magati ya kuhudumia majahazi na abiria yataboreshwa ikiwa ni pamoja na kushawishi uingiaji wa meli kubwa za kitali (cruise ships) zitakazo ongeza idadi ya watalii nchini na kuongeza pato la taifa.
Mwekezaji huyu, kwa mujibu wa makubaliano ya awali, atagharamia mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) katika Bandari zote (knowledge and skills transfer), ili hata kama atakuwa ameondoka baada ya mkataba, tuwe na wataalamu wetu wenyewe ambao wana uelewa na stadi za kutosha.
Manufaa mengine ni kuanzisha maeneo huru ya kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta zingine za kiuchumi zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi, utali, viwanda na biashara.
Ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam utakaotokana na uwekezaji wa DP World utasaidia pia kuchagiza ukuaji wa sekta ndogo za usafirishaji kwa njia ya reli (SGR, TAZARA na MGR) na barabara, na utaimarisha uhusiano wa kidiplomasia.
Kutokana na umuhimu huu, na kwa kuzingatia ushindani wa kibiashara hususan katika sekta ya bandari ambao tumekuwa nao dhidi ya ‘binamu zetu’ Kenya, kuna haja kubwa ya kuharakisha uwekezaji ili tuzikamate fursa hizi adhimu.
0629-29968