BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imesema inajivunia kuwa sehemu ya Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) uliozinduliwa hivi karibuni kwa safari ya kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.
Benki ya TCB imepewa heshima kuwa benki mdau namba moja katika mradi huo wa kimageuzi kwa kuwezesha mchakato wa kuagiza vichwa vya treni na mabehewa ya SGR na kutoa mikopo kwa wakandarasi wa Yapi Merkezi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TCB, Adam Mihayo akizungumza na waandishi wa habari jana, amesema lengo ni kuhakikisha kwamba wateja wanafikiwa na kunufaika na huduma za mradi wa SGR kupitia mawakala walioenea nchi nzima na uwezo mkubwa wa programu ya TCB Popote, wanamwezesha kila mmoja kujionea urahisi na uhakika wa usafiri wa kisasa.
Aidha, Mihayo anaeleza kuwa sambamba na hilo, benki ilishinda zabuni ya kutoa huduma za ukusanyaji wa nauli kwa njia za kidijiti ikiwamo kupitia mashine za kukatia tiketi (Ticket Vending Machine) hali kadhalika, programu ya simu ya TCB Popote inayomwezesha mteja kujifungulia akaunti kwa Sh. 1,000, inarahisisha ukataji wa tiketi za SGR mahala popote nchini.
“Wateja pia, wanaweza kununua tiketi zao bila usumbufu kwa mawakala 7,000 wa benki hiyo waliopo nchi nzima na hivyo kurahisisha upatikanaji wa tiketi na hivi sasa kadi za ATM zinaweza kutumika katika mifumo ya PoS na mashine za kukatia tiketi (TVM) zilizopo katika stesheni zote,” anasema.
Mihayo anasema katika kuwezesha mfumo kufanya kazi kwa ufanisi, Benki ya TCB imezindua mfumo wa malipo wa QR code kwa abiria ili kuwawezesha kutumia mfumo wa PoS bila kuhitaji intaneti kuzuia makosa ya kimfumo.
Aidha, anasem ubunifu wa mfumo wa kimawasiliano unaotumia akili mnemba kupitia mtandao wa WhatsApp unawezesha upatikanaji wa huduma za SGR kwa urahisi na kwamba , makusanyo ya manunuzi ya tiketi yameunganishwa na mfumo wa GePG ili kuendelea kujenga pato la nchi.
Benki ya Biashara Tanzania (TCB) ni taasisi ya kifedha inayoongoza katika utoaji wa usuluhisho wa kifedha unaolenga kukidhi mahitaji wa wateja wake na imekijipambanua katika uchumi jumuishi na maendeleo ya kiteknolojia, Benki ya TCB inajizatiti kuboresha huduma za kibenki na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini.