Baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi( CCM) Daniel Chongolo kuonesha kutofurahishwa na migogoro ya ardhi katika Jiji la Dodoma, hatimaye Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza kutafuta ufumbuzi ikiwa pamoja na kuitisha kikao cha wananchi.
Katibu Mkuu Chongolo akiwa katika ziara yake mkoani Dodoma akiwa Dodoma Mjini alipokea malalamiko ya kukithiri kwa migogoro ya ardhi, hivyo akaaagiza itafutiwe ufumbuzi wa haraka.
Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari na kitengo cha Mawasiliano Serikalini katika Wizara hiyo imesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula anatarajia kukutana na wananchi wa Dodoma kwa lengo mahususi ya kushughulikia changamoto ya mkwamo wa patikanaji hatimiliki za ardhi ndani ya Jiji hilo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kikao cha Dkt Mabula na Wakazi wa Jiji la Dodoma kitafanyika Juni 30, 2023 ambapo pamoja na mambo mengine kikao hicho kimelenga kutatua changamoto ya wananchi kushindwa kupata namba kwa ajili ya kufanya malipo ‘Control Number’
Pia mkwamo wa Wananchi kupata Hatimiliki ingawa wamekamilisha taratibu zote za Kupatiwa hati huku taarifa hiyo ikieleza mkutano huo wa siku moja umepangwa kufanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji Dodoma Mjini kuanzia Saa tatu kamili asubuhi.