
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, amesema kuwa serikali imejipanga kikamilifu kuboresha huduma za miundombinu na usafiri jijini, ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa barabara na huduma za mabasi yaendayo haraka ili kumaliza kero ya usafiri kwa wakazi wa jiji hilo.
Akizungumza katika ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na hali ya usafiri katika Kituo cha Mwendokasi Kimara mwisho, jana Julai 24,2024 jijini Dar es Salaam, Chalamila anasema kuwa barabara ya Bagamoyo inajengwa kwa ubora wa hali ya juu na Kampuni kutoka China, huku barabara ya Kimara ikijengwa na wakandarasi wazawa kutoka Tanzania wenye uzoefu.
Aidha, aliongeza kuwa huduma ya mabasi ya mwendo kasi (BRT) kupitia Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) inaendelea kuimarishwa, ambapo kwa sasa ujenzi unahusisha njia kutoka Mwenge hadi Ubungo kupitia Kimara, ikiwa na jumla ya Kilomita 13.2.
Chalamila alifafanua kuwa mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. bilioni 252 na kwamba unatekelezwa kwa fedha za ndani, jambo linaloonesha dhamira ya serikali kuboresha maisha ya wananchi bila kutegemea misaada ya nje.

“Barabara hizi si tu kwamba ni za kiwango cha juu, bali pia zinakuja na mpango mzuri wa mabasi mapya yenye huduma bora. Tumejipanga kuhakikisha si tu njia kuu zinapata usafiri, bali hata maeneo ya pembezoni yanaunganishwa,” alisema Chalamila.
Anabainisha kuwa, Zabuni kwajili ya kampuni zitakazotoa huduma za usafiri katika njia hizo imetangazwa na uteuzi wa kampuni mbili zimepatikana ambazo zimeshaanza kuagiza mabasi kwaajili ya kuanza kutoa huduma.
Chalamila anasisitiza kuwa, Serikali sikivu ya Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inafanya kazi kwa bidii kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa jiji la kisasa lenye usafiri wa haraka, salama na nafuu kwa wananchi wote.
Kuondoa watendaji wasiofaa
Chalamila anasema wameanza mchakato wa kuwaondoa watoa huduma wa sasa katika barabara kuu za mwendokasi, zikiwamo barabara ya Morogoro, kutokana na kushindwa kwa watoa huduma hao kwenye ufanisi ikiwamo kuongeza mabasi kwa wakati na kuendana na teknolojia inavyokuwa.
Chalamila anasema “Na ndiyo maana kwenye Barabara ya Morogoro na hii ambayo inaanza, hamjasikia nimetaja UDART (Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka), kwahiyo mtaelewa nini kimefanyika. Kwa lugha nyepesi ni kwamba tumeanza sisi wenyewe kujisahihisha, kwamba wewe bwana tulidhani unatoa huduma vizuri na una ‘commitment’ lakini tunaona hapana, ni kama unatunafikia ili Watanzania waendelee kulia.”
Naye Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Athuman Kihamia, amesema mabasi mapya yatakayoongezwa yatakuwa na viwango tofauti vya huduma ikiwa ni pamoja na huduma ya VIP Class kwa abiria watakaohitaji kulipia huduma ya juu.
Amesema tayari mwekezaji mpya ameshaagiza mabasi 99 ambayo yapo njiani na hadi kufika Agosti 30 mabasi 200 yatakuwa yameshawasili nchini na kuanza kufanyakazi kwenye barabara ya Mbagala.
Kero mwendokasi
Awali akiwa Kituo cha mwendokasi Kimara, Chalamila amefanya ukaguzi wa mwenendo wa usafiri na usafirishaji wa abiria.
Chalamila anaonesha kutoridhishwa na ufanyaji kazi wa mabasi hayo kwasababu yapo machache huku wenye mahitaji maalum kutokuwa na mazingira wezeshi ya kutumia usafiri huo.
Chalamila, anasema upungufu na kutokuboreshwa kwa mabasi hayo ni vitendo vya kuwahujumu wananchi wanaotumia usafiri huo ni hujuma dhidi ya juhudi za serikali hususan katika kuleta maendeleo na kuwahudumia wananchi.
Chalamila anasema tangu kuanzishwa kwa huduma hiyo takribani miaka tisa iliyopita, hakuna jitihada zozote zilizochukuliwa kuboresha au kuongeza mabasi, hali inayosababisha msongamano na kuchelewesha safari za wananchi.
Chalamila pia anahoji ni kwa namna gani mtu binafsi anaweza kutumia gari moja kwa miaka tisa mfululizo bila kufikiria kulibadilisha, achilia mbali magari ya umma yanayohudumia maelfu ya Watanzania kila siku.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alionya kuwa kama wahusika wa usimamizi wa huduma hiyo hawatabadilika na kuchukua hatua madhubuti mara moja, basi atapendekeza wachukuliwe hatua kali, ikiwamo kuondolewa kwenye nyadhifa zao.
Naye Meneja wa Operesheni kutoka Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), Daniel Madilu, alisema upungufu wa mabasi unatokana na uchakavu wa mabasi kwasababu mabasi yanayotumika kwa sasa yapo 60 pekee kati ya 200 yaliyoanza kufanya kazi 2015.
Aidha, alieleza kuwa mabasi mengi ni chakavu na yanashindwa kufanyiwa ukarabati kutokana na vifaa kuhitajika kuagizwa nchini China,
Anasema ili kumaliza usumbufu wa abiria kugombea usafiri, yanahitajika mabasi 300 ili wanatumiaji kutumia kwa usalama na uhakika.