Rais Mwinyi atembelea banda la Nishati Maonesho ya Sabasaba

Apatiwa elimu juu ya utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia

Wizara ya Nishati kuendelea kuweka mazingira mazuri kwa tasisi zake kutekeleza majukumu yake kikamilifu

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi, ametembelea Banda la Wizara ya Nishati kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba jijini Dar es Salaam.

Akiwa kwenye Banda la Wizara ya Nishati, Mwinyi alipokelewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Neema Chalila Mbuja, ambapo alimweleza juu ya hatua za utekelezaji zilizofikiwa kwenye utekelezaji wa mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya kupikia na kuongeza kuwa ajenda hiyo ni utekelezaji wa azimio la Rais Samia kama kinara wa nishati safi ya kupikia.

Alisema Wizara ya Nishati kupitia taasisi zilizopo chini ya Wizara zimekuwa zikitekeleza kwa vitendo ajenda hiyo kuunga mkono jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa nishati safi ya kupikia kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.

Wizara ya Nishati tayari imezindua mikakati miwili ya nishati safi ya kupikia na ule wa mawasiliano ili kuwezesha utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia kwa vitendo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *