Na Badrudin Yahaya
TIMU ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, imekata tiketi ya kushiriki michuano ya Afcon itakayofanyika mwakani nchini Morocco baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Guinea katika mechi ya mwisho ya hatua ya makundi iliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Bao pekee la Stars katika mchezo huo lilifungwa na winga wa kimataifa, Simon Msuva dakika ya 61 kipindi cha pili akiunganisha krosi safi kutoka kwa Mudathiri Yahaya.
Msuva amefunga bao lake la pili katika mechi ya pili mfululizo tangu aliporejeshwa kwenye kikosi kuelekea mechi iliyopita dhidi ya Ethiopia ambayo Stars walishinda 2-0 ugenini.
Guinea wakiongozwa na mshambuliaji wao nyota ambaye ni kinara wa mabao katika michuano hiyo, Serhou Guirassy, iliingia katika mchezo huu wakiwa nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kukusanya alama 9 na walijua wazi kuwa sare ya aina yoyote iliwatosha wao kufuzu.
Hata hivyo Stars ilionekana kuwa na njaa zaidi ya kupata ushindi lakini Msuva alipoteza nafasi mbili za kufunga mabao kipindi cha kwanza na kipindi cha pili.
Kwa upande wao, Guinea hawakuweza kutengeneza nafasi nyingi za wazi kutokana na uimara wa safu ya ulinzi wa Stars lakini kipindi cha kwanza walikaribia kufunga bao kama sio mpira alioupiga Mahmoud Hassan kugonga mtamba wa panya wakati akiwa analitazama goli.
Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Stars kutinga kwenye michuano ya Afcon baada ya kushiriki pia katika makala yaliyopita ambayo yalifanyika nchini Ivory Coast.
Mbali na rekodi hiyo lakini pia Stars inatarajia kuendelea kushiriki michuano hiyo kwa mara ya tatu mfululizo mwaka 2027 ambapo Tanzania itakuwa ni moja kati ya nchi mwenyeji wakishirikiana na Kenya na Uganda.
Mashindano ya Afcon ya nchini Morocco, yanatarajia kuanza Desemba 21 na kufika tamati Januari 18, 2026.
Kutokana na ushindi huo, kikosi cha Stars kinatarajiwa kuvuna shilingi milioni 500 kama motisha kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye aliwaahidi tangu mwanzo wa kampeni hizi za mechi za kuwania tiketi.