Na Zahoro Mlanzi
DAAH! Hatuna bahati! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, kuduwazwa kwa kufungwa mabao 2-0 na DR Congo katika mchezo wa kufuzu AFCON 2025, uliopigwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, umeifanya DR Congo kufuzu kwa fainali hizo ambazo zitafanyikia nchini Morocco ikiwa imejikusanyia alama 12 ikifuatiwa na Stars yenye alama 4 huku Guinea ikiwa na alama 3 na Ethiopia alama 1.
Guinea usiku wa kuamkia jana ilikuwa ugenini kuumana na Ethiopia katika mchezo mwingine wa kundi hilo H la michuano hiyo.
Mabao ya DRC katika mchezo huo, yalifungwa na mtokea benchi, Meshack Elia dakika ya 87 na katika dakika 5 za nyongeza na kufifisha matumiani ya Stars kucheza kwa mara nyingine fainali hizo.
Stars kama itataka kufuzu haina budi kushinda mechi zake mbili zilizobaki huku ikianza kuimbea mabaya Guinea kupata matokeo mazuri.
Katika mchezo huo ambao ulihudhiriwa na viongozi mbalimbali wa nchi akiwemo Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Stars ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga kipindi cha kwanza lakini Clement Mzize na Kibu Denis walishindwa kukwamisha mpira wavuni.
Moja ya tukio ambalo litabaki katika kumbukumbu za wapenda soka wengi ni la dakika ya 39 ambapo Kibu aliunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Mbwana Samatta na mpira kugonga mwamba na kutoka nje.
Lakini pia DR Congo nusura ifunge bao dakika ya 42 baada ya Simon Banza kupiga shuti nje ya eneo la hatari na kupanguliwa na Kipa, Ali Salum na kuwa kona tasa.
Katika dakika 45 za kwanza, DR Congo ilionekana muda mwingi kuwa nyuma ya mpira na kuipa nafasi Stars kushambulia lango lao ila tatizo lilikuwa katika umaliziaji.
Ukiachana na mabao ya haraka haraka yaliyofungwa na Elia, katika dakika tano za nyongeza, mtokea benchi, Fiston Mayele, nusura afunge bao baada ya shuti alilopiga kudakwa na Kipa Salum kutokana na shambulizi la kushtukiza walilofanya DR Congo.