Na Salha Mohamed, Dar es Salaam
KATIBU Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA), Dkt. Said Mohamed, amesema ufaulu wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2023 umeongezeka kwa asilimia 0.96, watahiniwa 31 sawa na asilimia 0.002 ya watahiniwa 1,356,392 wamefutiwa matokeo.
Mtihani huo uliofanyika Septemba, 2023 ukihusisha watahiniwa 1,397,293 waliosajiliwa kufanya mtihani, kati yao wasichana walikuwa 742,690 sawa na asilimia 53.15, wavulana 654,603 sawa na asilimia 46.85.
Dkt. Mohamed aliyasema hayo jana wakati akitangaza matokeo hayo akisema watahiniwa 1,092,960 sawa na asilimia 80.58 wamefaulu kwa kupata daraja A, B, C.
Wavulana waliofaulu ni 507,920 sawa na asilimia 80.59, wasichana 585,040 sawa na asilimia 80.58. Katika ubora wa ufaulu, watahiniwa wengi wamepata daraja B na C.
Waliopata daraja la B ni watahini 314,646 sawa na asilimia 23.20, daraja la C watahiniwa724,371 sawa na asilimia 53.41, watahiniwa 53,943 sawa na asilimia 3.98 wamepata daraja A.
Ubora wa wasichana kwenye ufaulu umeongezeka hadi asilimia 80.58 ikilinganishwa na asilimia 78.91 mwaka 2022, ongezeko katika daraja A ni asilimia 0.13, daraja B asilimia 0.96, daraja C asilimia 0.57.
Pia ubora wa ufaulu kwa wavulana umeongezeka hadi asilimia 80.59 ikilinganishwa na asilimia 80.41 katika mwaka 2022, daraja A asilimia 0.42, B asilimia 0.58, ufaulu wa daraja la C ukishuka kwa asilimia 0.83.
“Ufaulu wa wasichana na wavulana unafanana, wavulana wamefaulu kwa asilimia 80.59, wasichana 80.58, idadi ya shule katika makundi ya umahiri inaonesha kati ya shule zote 18,314 zenye matokeo ya PSLE 2023, shule 13,822 sawa na 75.47% zimepata Daraja C ikilinganishwa na madaraja mengine ya ufaulu,” alisema.
MASOMO YA LUGHA
Dkt. Mohamed alisema, ufaulu wa somo la Kingereza umeongezeka kwa asilimia 4.96 na ufaulu wa somo la Kiswahili umeshuka kwa asilimia asilimia 1.59.
Katika somo la Kingereza, ufaulu wa wavulana ni asilimia 34.39, wasichana asilimia 34.32 na somo la Kiswahili wasichana wanaufaulu mkubwa wa asilimia 88.91 ukilinganisha na wavulana asilimia 86.76.
Akizungumzia ubora wa ufaulu, alisema katika somo la Kiswahili umeongezeka kwa watahiniwa waliopata daraja la A hadi asilimia 30.44 ikilinganishwa na asilimia 29.96 mwaka 2022 licha ya asilimia ya watahiniwa waliopata daraja la B kupungua kwa asilimia 2.01.
Somo la Kingereza, ubora wa ufaulu umeongezeka kwa watahiniwa waliopata daraja A na B hadi asilimia 11.40 ikilinganishwa na asilimia 8.65 mwaka 2022.
HISABATI NA SAYANSI
Ufaulu wa Somo la Sayansi, Teknolojia ni silimia 74.08 na somo la hisabati asilimia 48.83. katika somo la Sayansi na Teknolojia umepanda kwa asilimia 2.45 na Hisabati umeshuka kwa asilimia 4.46 ikilinganishwa na 2022.
Katika Somo la Sayansi na Teknolojia, wavulana wana ufaulu wa asilimia 75.78, wasichana asilimia 72.60, Somo la Hisabati wavulana wana ufaulu wa asilimia 52.45 ukilinganisha na wasichana asilimia 45.69.
MATOKEO YAZUILIWA
Dkt Mohamed alisema, Baraza limezuia matokeo ya watahiniwa 360 waliopata matatizo ya kiafya, kushindwa kufanya Mtihani kwa masomo yote au idadi ya masomo.
Watahiniwa husika wamepewa fursa ya kurudia mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi (PSLE) mwaka 2024 kwa mujibu wa kifungu cha 32(1) cha Kanuni za Mitihani.
MATOKEO YAFUTWA
Dkt. Mohamed alisema Baraza limefuta matokeo yote ya watahiniwa 31 sawa na asilimia 0.002 ya watahiniwa 1,356,392 waliofanya mtihani.
Watahiniwa hao wamebainika kufanya udanganyifu katika mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi 2023 kwa mujibu wa Kifungu 30(2)(i) na (j) cha sheria cha Baraza la Mitihani Sura ya 107.
VITUO VYAFUNGIWA
Baraza limevifungia vituo vya mitihani viwili ambavyo ni Twibhoki (PS0904095) na Graiyaki (PS0904122) Halamshauri ya Serengeti, mkoani Mara.
Vituo hivyo vimethibitika kupanga kufanya udanganyifu katika mitihani hiyo kwa mujibu wa Kifungu 4(48) cha Kanuni za Mitihani 2026 hadi baraza litakapojiridhisha kuwa ni salama kwa uendeshaji mitihani ya taifa.
VITUO VYAPEWA ONYO
alisema baraza limeziandikia barua za onyo vituo vinne vya mitihani ambavyo ni Mother of Mercy (PS0203133), St. Marys Mbezi Beach Modern (PS0203088) katika Halamshauri ya Kinondoni, Dar es Salaam.
Vingine ni Charm Modern (PS0103111) Halmashauri ya Karatu mkoani Arusha na Morotonga (PS0904042) cha Halmashauri ya Serengeti, mkoani Mara.
“Vituo hivyo vilijaribu kujihusisha na vitendo vya udanganyifu katika mitihani, vitakua chini ya uangalizi wa Baraza hadi litakapojiridhisha ni vituo salama kwa uendeshaji wa mitihani ya taifa,” alisema.